Katambi aonya wasiopeleka michango hifadhi ya jamii

NAIBU Waziri Ofi si ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi amewataka waajiri kote nchini kuhakikisha wanalipa michango na tozo mbalimbali kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya WCF, PSSSF na NSSF.

Katambi alisema hayo juzi baada ya kutembelea mabanda ya mifuko hiyo ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Viwanja vya Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa.

Agizo la Katambi linakuja ikiwa ni wiki chache tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutoa maelekezo wakati akitoa hotuba ya kuahirisha kikao cha Bunge la Bajeti kuwa ifikapo Septemba 30, mwaka huu, waajiri kote nchini kutoka sekta ya umma na binafsi wahakikishe wanalipa michango na tozo mbalimbali kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Advertisement

“Agizo kwa waajiri wote nchini, iwe ni mamlaka za serikali, iwe ni watu binafsi hakikisheni mnapeleka michango, iwe ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), PSSSF au NSSF, mlipe kwa wakati vinginevyo tutachukua hatua kali za kisheria,” alionya Katambi.

Alisema kila mwezi mamlaka za serikali zinatengewa bajeti ya kutekeleza wajibu huo wa kisheria kuwasilisha michango, hivyo wanao wajibu wa kuhakikisha wanalipa michango hiyo kwa wakati. “Kwa sekta binafsi mtu ambaye hawasilishi michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ukimfuatilia vizuri ni mkwepa kodi pia, kwa hivyo inabidi tuwajue vizuri na ikibidi tutawatangaza,” Katambi.

Aliwapongeza watendaji wakuu wa mifuko hiyo, Dk John Mduma (WCF), Hosea Kashimba (PSSSF) na Masha Mshomba (NSSF) kwa kuleta mapinduzi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. “Kwa kweli Rais anaona mbali sana, hawa wakurugenzi ni watu wa aina yake, wameleta mapinduzi makubwa kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii, niliwahi kuwakaribisha wageni kutoka Kenya waliokuja kujifunza masuala ya hifadhi ya jamii kwa kweli wameshangaa ubora wa huduma zinazotolewa na mifuko hii,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Wakurugenzi Wakuu wa mifuko hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dk John Mduma alisema mifuko yote iko vizuri na itaendelea kutoa huduma kwa weledi katika kukusanya michango na kutoa mafao, majukumu ambayo wamekabidhiwa na serikali kuyasimamia.

“Nataka niwahakikishie kuwa tutaendelea kuimarisha eneo la Tehama, ulimwengu sasa unatoa huduma kwa njia ya kidijiti, mifuko yote inawekeza kwa kasi ili kuhakikisha sehemu kubwa ya kazi zetu zinatolewa kwa njia ya mtandao ili kupunguza gharama kwa wateja wetu wawe ni waajiri au wafanyakazi wanaofuatilia mafao yao,” alisema Dk Mduma.

Katambi alifuatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEA), Juma Buruhani Mohammed ambaye alisema amefarijika kupata fursa ya kujionea shughuli za mifuko hiyo.

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *