Katambi atoa maelekezo ukaguzi mipakani

ARUSHA: Naibu Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Ajira na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi amewaagiza wanaotoa huduma eneo la Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani (OSBP) cha Namanga na Kenya kuhakikisha wanarahisisha huduma za ukaguzi kwa abiria, magari na mizigo ili kuokoa muda na kudhibiti wanaosafirisha watoto ikiwemo watu watu wenye ulemavu

Pia amesisitiza ulipwaji wa kodi ni muhimu ili serikali iweze kupata mapato sanjari na Idara ya Uhamiaji kudhibiti watu wenye nia ovu ambao hutumia watoto na watu wenye ulemavu kuwapitisha maeneo ya mipakani.

Advertisement

Katambi ametoa rai hiyo leo wilayani Longido eneo la mpaka wa Namanga wakati alipofanya ziara ya kukagua utoaji huduma mpakani hapo na kuangalia haki za abiria na watu wenye ulemavu .

Amesisitiza huduma za pamoja kuimarishwa zaidi ikiwemo kubaini watu wanaosafirisha binadamu unaofanyika maeneo ya mipakani ikiwemo wale wanaotumia fursa za kusafirisha watoto na watu wenye ulemavu kwenda nchi nyingine kuwatumikisha.

“Serikali imewekeza fedha nyingi katika kituo hiki na vifaa vya kisasa vimewekwa turahisishe utoaji huduma ikiwemo kaguzi zaidi kwenye malori, mabasi na abiria lakini dhibitini wanaotumia njia za panya ”

Naye Mfawidhi wa kituo cha Uhamiaji mpaka wa Namanga ,Gulugu Nkanga amesema sheria ya nchi za EAC  zinaruhusu raia wa mpakani wa nchi zote mbili kuvuka mpaka bila kuwa na hati za kusafiria ndani ya kipenyo cha kilomita 20.