KATAVI: Maandalizi Sensa yafikia asilimia 98

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko

ZIKIWA zimebaki siku mbili kuelekea siku ya Sensa ya watu na makazi nchini, Mkoa wa Katavi umefika asilimia 98 ya maandalizi ya zoezi hilo,hiyo ikiwa ni ishara kuwa wananchi wa Mkoa huo wako tayari kuhesabiwa ifikapo Agosti 23 mwaka huu.

Akizungumza na wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe katika bonaza lililoandiwa kwa ajili ya kutoa elimu na kuhamasisha Sensa, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema mafanikio hayo ni kutokana na ushirikiano baina ya viongozi,kamati za Sensa pamoja na wananchi.

Akitoa elimu kuhusu Sensa, RC Mrindoko alisema anayetakiwa kuhesabiwa ni mtu yoyote aliyelala ndani ya mipaka ya Tanzania siku ya kuamkia tarehe ya Sensa.

Advertisement

“Maandalizi kuhusu zoezi hili yamekamilika kwa asilimia zaidi ya 98 ndani ya Mkoa wa Katavi,na kwa maana hiyo tunasubiri tu siku ifike na Sensa ifanyike”

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geoffrey Pinda alisema wanapata changamoto wanapoomba fedha za maendeleo katika majimbo yao kutokana kutojua idadi halisi ya wananchi wao hivyo zoezi hilo limekuja muda muafaka na ni muhimu sana hasa katika mikoa ambayo inachipukia kimaendeleo.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geoffrey Pinda

“Kwenye kuomba msaada wa maendeleo kwenye Jimbo,shida kubwa ukiulizwa mko wanapi? unataja idadi ya mwaka 2012, wakati sasa hivi kuna mwingiliano na watu wameongezeka, tutawatambua wote na itatusaidia sana katika mipango ya maendeleo” Alisema Pinda.