Katavi, Manyara na Tabora vinara kujisaidia vichakani
DAR ES SALAAM: MIKOA ya Manyara, Katavi na Tabora inaongoza kwa wakazi wake kujisaidia vichakani kutokana na kushika nafasi za chini katika takwimu za hali ya matumizi ya vyoo bora kwenye mikoa yote Tanzania bara.
Kwa mujibu wa takwimu hizo Tabara inashika nafasi ya 26 ambapo Kaya wanaotumia choo bora bila ya kutumia na kaya nyingine ni asilimia 33.6, Kaya zaidi ya moja wanaotumia bora choo ni asilimia 6.9 asilimia ya watu wasiokua na vyoo ni 21.9.
Katavi inashika nafasi ya 25 ikiwa na watu wa kaya moja kutumia choo bila ya kuchangia na kaya nyingine ni asilimia 42.2, watu wanaochangia choo bora zaidi ya kaya moja ni asilimia 10.3, watu wasiokuwa na vyoo ni asilimia 24.3 wakati Manyara inashika nafasi ya 24 ikiwa na asilimia 46.1 ya watu wanaotumia choo bora bila kuchangia na kaya nyingine, asilimia 7.8 wanachangia choo zaidi ya kaya moja na asilimia 22.8 hawana vyoo.
Kufuatia hali hiyo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 9.8 ya watu nchini hawana vyoo kabisa ambapo hali ni mbaya zaidi maeneo ya vijijini.
“Kwa mujibu wa taarifa hii asilimia 13.4 ya wakazi wa vijijini hawana vyoo kabisa. Tafsiri ya kiashiria hiki ni kwamba watu hawa ndiyo wanaojisaidia ovyo vichakani na maeneo mengine ambayo sio rasmi.
“Hali hii inachangia kuwepo kwa magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu ambapo kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba 2023 jumla ya watu 749 waliougua na 16 kupoteza Maisha”. Amesema Ummy.
Aidha, ameziagiza sekretatarieti za mikoa na halmashauri kuhakikisha kaya zote nchini zinakuwa na vyoo bora.
Pia, amezielekeza kufanya ukaguzi kwenye kaya, sehemu za jumuiya, maeneo ya biashara na taasisi zote kwa kuhakikisha zinajenga na kutumia vyoo bora.
“Simamieni vyema sheria ya afya ya Jamii na Sheria ndogo zinahusiana na ujenzi na matumizi ya choo bora kwenye ngazi ya Kaya, Taasisi na maeneo ya Jumuiya,”amesema.
Vile vile ameelekeza kuhakikisha zinasimamia vyema matumizi ya vyoo kwa wasafiri wawapo safarini kwa kuhakikisha mabasi yanasimama kwenye maeneo rasmi ikiwemo stendi za mabasi na vituo maalum pamoja na kupiga marufuku tabia ya wasafiri kujisaidia hovyo maarufu kama kuchimba dawa kwani ni aibu kwa Taifa na pia udhalilishaji wa utu.