Katibu Mkuu asifu utekelezaji wa miradi TSN
KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Teknolojia na Mawasiliano ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla amepongeza utendaji kazi wa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Tuma Abdallah sambamba na watendaji wa kampuni hiyo kwa uchapaji kazi.
Katibu Mkuu huyo pia amesifu utekelezaji wa mradi wa mabilioni ya fedha za Serikali ulioelekezwa katika ujenzi wa kiwanda cha uchapaji jijini Dar es Salaam na kusimika mitambo mipya ya uchapaji kibiashara ili kuweza kuongeza mauzo ya magazeti na machapisho mengine.
Akizungumza leo Mei 30, 2023 katika ziara yake ya kwanza ya kikazi katika makao Makuu ya TSN, Tazara Katibu Mkuu amesema ameshuhudia maandalizi ya ujenzi wa ofisi kubwa ya kampuni hiyo sambamba na kujionea mitambo na mashine za kisasa za uchapishaji zilizowasili ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo.
“Nimefanya vikao na kurugenzi (management) ya kampuni hii wamenieleza changamoto zao, mimi kama mtendaji nimezichukua, pia nimejionea mimi mwenyewe ile fedha ambayo serikali imewekeza tayari baadhi ya vifaa vimeshawasili na maandalizi ya ujenzi yanaendelea kufikia mwishoni mwa mwaka huu nategemea ujenzi kukamilika.”
Mbali na hayo ameipa changamoto Kurugenzi ya TSN kuanzisha gazeti maalumu kwaajili ya kufundisha na kukuza lugha adhimu ya Kiswahili barani Afrika.
“Leo nilitoa maelekezo kwamba kwa sababu Kiswahili kinakua na nchi nyingi zimeanza kufunguka kutaka kujifunza Kiswahili, sasa nikawapa changamoto nikasema badala ya kutoa magazeti ya Daily News, Habari Leo kwanini tusitoe gazeti la Afrika ili kufundisha Kiswahili kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.”
Itakumbukwa utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa bajeti uliosomwa katika hotuba ya bunge la bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambapo iligusia ujenzi wa kiwanda cha uchapaji jijini Dar-es-salaam na kusimika mitambo mipya ya uchapaji kibiashara ili kuweza kuongeza mauzo ya magazeti na machapisho mengine.