KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli kesho atazindua benki ya kisasa ya mbegu yenye uwezo wa kuhifadhi mbegu kwa miaka 100 inayomilikiwa na Taasisi ya Utafiti na Uendelezaji wa Mazao ya Mbogamboga Duniani (WVC).
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk Gabriel Rugalema amesema benki hiyo kubwa ya kisasa Afrika inaweza kuinua uchumi wa Mkoa wa Arusha na Afrika kwa ujumla kwani ndio malengo yaliyokusudiwa na katika kukuza kilimo cha mboga mboga Tanzania na Afrika.
Alisema karne ya kizazi kijacho inaweza kupata na kusikia historia mbegu mbalimbali kama vile mchicha lishe, ngogwe na mbegu mbalimbali kutoka na benki hiyo kuwa na vifaa vya kisasa vya kuhifadhi mbegu kwa muda huo.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa vizazi vya sasa vimeweza kuona mbegu ya mboga mboga iliyohifadhiwa mwaka 1997 katika kituo hicho na kizazi kijacho kitapata kuona na kusikia mbegu ya mbogamboga iliyohifadhiwa mwaka huu katika muda huo.
‘’Benki hiyo imejengwa katika jengo jipya, vifaa vya kisasa na ina uwezo wa kuhifadhi mbegu kwa karne moja ni faida kwa kizazi kijacho kujua historia ya mbegu ya mbogamboga,’’ alisema Rugalema
Mtaalamu na mtafiti wa mbegu kutoka benki ya kituo hicho, Dk Abdul Shango alisema kuwa uzinduzi wa benki hiyo unaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuinua uchumi wa wakulima wa mbogamboga katika Mkoa wa Arusha na Kanda ya kaskazini kwa ujumla
Shirika la Chakula Duniani (FAO) limesaini makubaliano ya awali na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendeshaji wa Kilimo cha Mboga Mboga za Asili za Majani ,Kurugenzi ya Mashariki na Kusini Mwa Afrika ya Mkoani Arusha yenye lengo la kuboresha kilimo hicho nchini na Afrika na kuipatia taasisi hiyo Dola Kimarekani 650,000 sawa na Sh bilioni 1.6.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Usimamizi wa Mikataba ya Kimataifa ya FAO, Uhifadhi wa Vinasaba vya Mbegu, Dk Kent Nnadozie katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo hafla iliyofanyika katika ofisi ya WVC Tengeru nje ya jiji la Arusha na kuhudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Uzalishaji Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Beatrice Banzi pamoja na watumishi wa taasisi hiyo na viongozi wengine wa serikali mkoani Arusha.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Katibu Nnadozie alisema lengo la FAO kukabidhi fedha hizo kwa taasisi hiyo ni kutaka kukuza na kuboresha kilimo cha mbogamboga hapa nchini na Bara la Afrika kwani kilimo hicho kinaweza kukuza uchumi wa nchi za Afrika hususani nchi wakulima wa mazao hayo.
Dk Nnadozie alisema lengo lingine la FAO ni kutaka kukuza Benki ya Mbegu katika taasisi ya WVC ya Arusha kwani benki hiyo ina aina 7,000 za mbogamboga katika benki yake wakati duniani kuna aina milioni 1 za mbegu za mbogamboga.
Alisema ni wajibu wa WVC kujikita katika kuboresha na kukuza kilimo cha mbogamboga nchini na Afrika ikiwa ni pamoja na kwenda sambamba kuongeza jitihada katika kuongeza idadi ya mbegu katika benki yake kwa faida ya baadae kwani aina iliyopo bado haitoshi kukuza uchumi wa nchi na Afrika.
‘’FAO ina lengo la kukuza kilimo cha mbogamboga nchini na Afrika pia ina lengo la kukuza uzalishaji wa mbegu katika Benki ya WVC kwani duniani kuna aina ya mbegu milioni 1 lakini WVC katika benki yake ina aina 7,000 tu ya mbegu hatua ambayo alisema haitoshi,’’ alisema Nnadozie
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa WVC, Dk Gabriel Rugalema kwanza ameishukuru FAO kwa msaada huo wa fedha na kusema kuwa fedha hizo zinaweza kutatua baadhi ya changamoto zilizokuwa zikikwamisha jitihada za taasisi hiyo.