Katibu Mkuu mpya UVCCM atema cheche

SONGWE; KATIBU Mkuu mpya wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM ),  Fakii Lulandala amewataka viongozi wa UVCCM katika mikoa yote kujenga tabia ya kuwatembelea vijana katika shughuli zao, ili kubaini changamoto zinazowakumba bila kujali itikadi za vyama.

Amesema hayo wakati anazungumza na vijana wa UVCCM  Mkoa wa Songwe waliompokea kwa shangwe, wakati akikabidhi ofis ya ukuu wa wilaya kwa Mkuu wa Wilaya mpya Kenan Kihongosi, nafas aliyokuwa akihudumu katika Wilaya ya Momba.

Amesema ili kujenga chama kilicho imara ni lazima kuwe na vijana imara ,wazalendo na wachapakazi ambao watakitetea muda wote.

” Natoa rai kwa viongozi kuanzia kwenye mashina mpaka ngazi ya mkoa kuandaa program maalumu ya kuwatembelea vijana kuanzia ngazi ya chini mpaka mkoa kuangalia changamoto zinazowakumba vijana katika jitihada za kujikwamua kiuchumi,” amesema.

Amesema ripoti za changamoto za vijana zikikusanywa zitapelekwa ngazi ya juu kwa ajili ya utatuzi na kuwasaidia zaidi vijana  kusonga mbele na kuimarika kiuchumi.

Akikabidhi ofisi kwa Kihongosi,  Lulandala alisema wilaya hiyo upande wa Kaskazini Magharibi inapakana na  Zambia, hivyo kumuomba Mkuu wa Wilaya kuendelea kudumisha ujirani mwema na Mkuu wa Wilaya ya Nakonde upande wa Zambia.

Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Songwe, Fatuma Hussein alisema wamepokea maelekezo yaliyotolewa na kiongozi huyo ngazi ya Taifa ili kuwakwamua vijana ambao ndio tegemeo la nchi.

“Bahati nzuri ndani ya mkoa wetu vijana wengi wanaonufaika na fursa mbalimbali huwa hatuangalii itikadi zao za vyama, ” alisema Fatuma.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Momba, Kenan Kihongosi baada ya kukabidhiwa ofis alisema atayaendeleza mazuri yote aliyoyaanzisha mtangulizi wake na kuwataka wakuu wa idara kuhamia Momba, ili kuwahudumia wananchi kwa ukaribu zaidi.

Habari Zifananazo

Back to top button