Katimba acharuka wakandarasi wanaochelewesha miradi

KIGOMA: NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Zainabu Katimba ametaka wakandarasi wanaochelewesha miradi mbalimbali inayotekelezwa mkoani Kigoma bila kuwa na sababu muhimu kuchukuliwa hatua kulingana na sheria na taratibu za mikataba yao.

Katimba amesema hayo alipofanya ziara ya kiserikali mkoani Kigoma kutembelea miradi ya barabara ukiwemo mradi wa kuendeleza na kuboresha Miundombinu ya Miji  Nchini Tanzania ( TACTICS)  Manispaa ya Kigoma/Ujiji unaotekelezwa kwa mkopo kutoka benki ya Dunia.

Amesema kuwa hakubaliani na taarifa ya Mhandisi Mshauri wa mradi huo, John Meena inayoeleza kuwa mradi huo hadi sasa umetekelezwa kwa asilimia 17 wakati ulipaswa kuwa umefika asilimia 35 na kwamba sababu ya uwepo wa mvua nyingi hazina msingi kwa sababu kazi iliyokuwa ikianza haikuwa inaathiriwa na mvua kwa kiasi cha kusimamisha mradi.

Akiwa kwenye ziara hiyo Katimba ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya barabara chini ya Wakala wa barabara mjini na vijijini Mkoa Kigoma (TARURA) na kuitaka taasisi hiyo kuwa wakali kwa wakandarasi ambao hawatekelezi shughuli zao kwa mujibu wa miakataba yao.

Awali mhandisi Mshauri wa mradi huo, John Meena kutoka kampuni ya Saba Engineering alisema kuwa kwa sasa mradi huo upo asilimia 17 nyuma ya utekelezaji ikiwa unapaswa kuwa asilimia 35 na kwamba mvua nyingi zimesababisha mradi kuchelewa.

Katika ziara hiyo Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa Kigoma, Alias Mutapima alimtembeza Naibu Waziri wa TAMISEMI kwenye barabara mbalimbali zilizotekelezwa kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024  ikiwemo barabara zilizojengwa kwa zege katika maeneo ya miinuko ili kukabiliana na uharibifu wa barabara hizo wakati wa Mvua nyingi na madaraja ya mawe.

 

Habari Zifananazo

Back to top button