DAR ES SALAAM: MKURUGENZI Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo) ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema kauli ya Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro juu ya ukaguzi wa hati ya kusafiria ‘passport’ kwa mashabiki viwanjani ilikuwa ni utani wa kimichezo na wala si msimamo wa serikali.
Amesema hayo leo Dar es Salaam wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari na wahariri,baada ya kuzungumzia mafanikio ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akijibu swali kuhusu ni ipi kauli ya serikali kuhusu mashabiki kuingia uwanjani na hati ya kusafiria, kutokana na kauli ya Dk Ndumbaro kusema watakaoingia uwanjani na jezi za timu pinzani watakaguliwa hati za kusafiria ili kuthibitisha uraia wao.
Kauli hiyo aliitoa kuelekea michezo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) itakayopigwa Aprili 29 na 30, ikihusisha vilabu vya Simba SC vs Al Ahly ya Misri, wakati mchezo mwingine utazikutanisha Yanga SC vs Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
“Ni kawaida kwenye michezo timu shindani zinapocheza kauli za kutambiana hutolewa na asilimia 80 ya kauli hizo ni majigambo tu ya kimichezi na si kauli rasmi,”amesema Matinyi.
Amesema chombo chenye mamlaka ya ukaguzi wa Hati ya Kusafiria ni Idara ya Uhamiaji ambao shughuli hiyo huifanya kwa weledi na uadilifu mkubwa.
Hata hivyo, Matinyi ameyaasa mashirikisho ya mpira wa miguu nchini na yale ya kimataifa kutoyapa nafasi maelezo yoyote ya upotoshaji kwani dhumuni la Waziri Ndumbaro ni kusisitiza mashabiki wa michezo nchini kujikita zaidi katika uzalendo ikiwemo kushabikia zaidi vya ndani.