SIKU moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuahidi kutafuta suluhu ya malalamiko ya kikokotoo, baadhi ya wastaafu wameibuka na kutoa ushauri unaotaka iundwe tume maalumu itakayoshughulikia suala hilo wanalotaka lifutwe kabisa.
Pamoja na tume hiyo wastaafu hao wamemshauri Rais kuivunja bodi inayounda Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ili kuruhusu baadhi ya wastaafu kuwa wajumbe wake na kama ukwasi wa mfuko huo unaendea kushuka, basi utaratibu wa ukusanyaji wa michango ya wanachama na ulipaji wa mafao, urudishwe Hazina Kuu ya serikali.
Wakizungumza na wanahabari leo, wastaafu hao wamegusia pia ombi lao kwa serikali linalotaka wastaafu wapewe nyongeza ya pensheni yao ya kila mwezi na kuwe na min pensheni kwa wastaafu wote.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Mkoa wa Iringa, Stanslaus Muhongole amesema bodi ya PSSSF haina wajumbe wastaafu wa kutosha jambo linalozorotesha masuala mbalimbali yanayohusu stahiki za wastaafu kufanyiwa kazi kwa ufanisi.
“Kukiwa na wastaafu wa kutosha katika bodi ya mfuko huo tunaamini malalamiko mengi ya wastaafu yatafanyiwa kazi kwa kuzingatia maslai mapana ya kundi hilo,” alisema.
Muhongole alisema wamemsikia Rais akizungumzia kushuka kwa ukwasi wa mifuko ya jamii na kama hali ndiyo ameshauri maswala yanayohusu hifadhi ya jamii yaondolewe katika mifuko hiyo na kupelekwa Hazina ya serikali.
Naye Mratibu wa Mkoa wa Iringa wa Umoja wa Wastaafu Tanzania, Peter Mvilli amezungumzia nyongeza ya pensheni ya wastaafu akisema ni kilio kikubwa kwa wastaafu.
Mvilli alimshukuru na kumpongeza Rais Dk Samia kwa ahadi yake ya kuyafanyia kazi malalamiko ya kikokotoo huku akiomba serikali iangalie uwezekano wa kutoa nyongeza ya pensheni kwa wastaafu.
“Kama nyongeza ya pensheni hiyo imewezekana kufanywa kwa asilimia 100 na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tunaamini inawezekana pia kwa serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Mmoja wa wastaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania, Stafu Sajenti Augustino Sambagi ambaye ni Katibu wa Wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Mkoa wa Iringa alisema wakati akistaafu zaidi ya miaka 20 iliyopita pensheni yake ilikuwa Sh 73 na kwa kipindi chote hicho imepanda na kufikia Sh 100,000 na zaidi.
“Siku zote tumekuwa tukiahidiwa kuongezewa lakini ahadi hiyo haitekelezeki.
Wanajeshi wenzangu wastaafu zaidi ya 300 walioko mkoani hapa, wamenituma niiombe serikali itukumbuke,” alisema na kuzungumzia Sh 100,000 anayopata hivisasa isivyowiana na gharama za maisha ya sasa.
Alimuomba Rais Dk Samia kukifanyia kazi kilio chao ili kuwanusuru wastaafu wa jeshi kujiingiza katika magenge ya uhalifu kwa lengo ka kupata ziada inayoweza kuwasaidia kumudu maisha yao.