Kaya 2000 Sangara zachekelea huduma za maji

MANYARA: KAYA 2000 za kijiji cha Sangara kilichopo mkoani Manyara zimenufaika na matumizi ya dira za maji za malipo ya kabla ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya maji pamoja na kudhibiti kuvuja maji kunakosababisha hasara kwa mteja.

Kijiji hicho kimenufaika na Shirika la WaterAid ambalo liliingia ubia na kampuni ya EwaterPay na kufunga mita hizo za malipo ya awali.

Pia, kupitia mradi wa maji wa vijiji vitano wilaya ya Arumeru mkoani Arusha WAterAid imefunga mita za maji za malipo ya kabla na kufikia takribani wananchi 23,000.

Akizungumza leo Mei 23, 2023 mkoani Arusha, Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la WaterAid Tanzania, Anna Mzinga amesema kupitia miradi hiyo miwili, mwananchi anauwezo wa kujaza pesa katika simu yake ili kulipia tokeni maalumu inayotumika kuchotea maji na kwa kiasi cha Sh 30 kupata ndoo moja ya maji ya lita 20, fedha ambayo huingia moja kwa moja kwa kikundi cha watumia maji (CBWSO).

Amesema, Shirika limeendelea kujifunza namna ya kuboresha ubunifu huu kutoka mradi mmoja kwenda mwingine, ambapo miradi mingine iliyotekelezwa kwa kuiga ubunifu huu ni pamoja na mradi wa bwawa la maji Kwamaizi na Itigi Singida.

“Tunaipongeza Serikali kwa kuasili mfumo huu, sisi kama Shirika tunaamini sana katika ubunifu na ni moja ya nyenzo muhimu tunayotumia katika kutekeleza na kuwasilisha miradi yetu,”amesema Anna na kuongeza

“Tutaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kubuni miradi mipya inayotumia teknolojia na kuifanyia tathmini zitakayorahisisha kujifunza na hatimaye kuleta matokeo chanya ya upatikanaji wa maji hasa katika kumtua mama ndoo kichwani nchini Tanzania” Amesema

Amesema, hivi sasa moja ya malengo iliyojiwekea, WaterAid Tanzania imepanga kujikita kimkakati katika Wilaya ya Hanang, mkoani Manyara katika kipindi cha utekelezaji wa mpango mkakati.

 

Habari Zifananazo

Back to top button