Kaya zenye uhitaji Iringa kupewa chakula

WAKALA wa Hifadhi ya Chakula Taifa (NFRA), imeridhia kupeleka tani 130 za chakula cha dharura zitakazosambazwa katika halmashauri ya wilaya ya Iringa, ili kunusuru kaya zinazokabiliwa na tatizo njaa.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya baraza la madiwani la halmashauri hiyo kuzungumzia uwepo wa kaya zenye njaa katika halmashauri yao na kuipigia magoti serikali isaidie kuzinusuru na shida hiyo.

Akizungumza na wanahabari leo, Ofisa wa NFRA wa kanda ya Makambako, Steven Lihapa alisema wamepokea maombi hayo na wamekamilisha taratibu za kusambaza chakula hicho.

“Tumeshakamilisha taratibu zote, kuanzia kesho Februari 25 chakula hicho kitaanza kufikishwa katika kata zenye uhitaji,” alisema.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Steven Mhapa aliishukuru serikali kwa kushughulikia tatizo hilo mapema, akisema pamoja na ahadi hiyo ya NFRA mahitaji ya chakula cha dharura ni mkubwa kwani kata nyingi zimekumbwa na tatizo la njaa.

Alisema tani 130 zilizotolewa na NFRA zitasaidia kunusuru kaya zilizo katika hali mbaya zaidi.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,  Isdori Karia alizitaja kata zitakazoanza kunufaika na msaada huo wa chakula kuwa ni pamoja na Nzihi, Malengamakali, Izazi, Kiwele, Migori, Kihorogota, Nyang’oro na Mlowa.

Karia ambaye pia ni Ofisa Kilimo wa halmashauri hiyo alisema wanaendelea kupokea maombi ya uhitaji wa chakula hicho kutoka katika kata mbalimbali na kuziwasilisha kwa NFRA, ili kupunguza changamoto hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button