Ken Gold waamua kuja kivingine

UONGOZI wa timu ya soka ya Ken Gold umesema baada ya kumalizika kwa ligi daraja la kwanza(Championship) sasa unatarajia kujipanga upya kwa kuvunja kikosi chote pamoja na benchi la ufundi.

Mkurugenzi wa timu hiyo, Keneth Mwambungu amesisitiza kuwa anataka kufanya maboresho makubwa katika timu hiyo kuelekea msimu ujao wa ligi ya Championship.

Mwambungu alisema uamuzi wa kuvunja kikosi hicho na benchi lake la ufundi unatokana na tathimini iliyofanyika baada ya kumalizika ligi na kubaini mapungufu mbalimbali, hivyo wanaanza kuyafanyia kazi mapema.

Alisema uongozi unatambua ugumu wa ligi daraja la kwanza baada ya kuwa na uzoefu wa misimu mitatu iliyoshiriki pasipo kupata mafanikio ya kupanda daraja, hivyo kuna haja ya kujipanga upya.

“Unajua ligi daraja la kwanza ni ngumu sana, tumecheza huu msimu wa tatu sasa, navunja kikosi chote pamoja na benchi la ufundi,tunaanza upya,” alisisitiza Mwambungu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa KenGold, Benson Mkocha aliongeza kuwa baada ya kushindwa kufikia malengo ya kupanda ligi wameona waanze upya, ambapo hivi karibuni wataanza kutangaza utaratibu wa namna gani watafanya usajili.

“Uongozi umeona kuwepo kwa sababu ya kujipanga na kuanza upya baada ya kushiriki misimu mitatu bila mafanikio yaliyotarajiwa. Tunajipanga tutatangaza hivi karibuni utaratibu tutakaoutumia kusajiLi upya,” Alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button