Kenya yapata soko la parachichi China

Kenya yapata soko la parachichi China

MAPARACHICHI kutoka Kenya yamepata soko kubwa nchini China kutokana na ubora wake unaozidi kuwavutia watu wengi duniani kwa kuwa yanafaa kupondwapondwa na kuwekwa kwenye mkate unaotumika kote duniani na kusababisha mahitaji yake kuzidi kuongezeka.

Asilimia kubwa ya wateja wa maparachichi kutoka Kenya ni Wachina ambao wamebainisha kuwa ladha ya bidhaa hiyo ni tofauti na ile inayoingizwa nchini kwao kutoka katika mataifa yanayotumia mfumo wa kuyagandisha kwenye friji.

Kwa muda mrefu Kenya imejaribu kupeleka matunda hayo China bila kuyagandisha lakini China ilikuwa ikiruhusu matunda yale tu ambayo yamegandishwa kwenye friza kwa sababu ya hofu ya magonjwa yanayosambazwa na nzi.

Advertisement

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kilimo Kenya, Chris Flowers, alisema Ulaya na Mashariki ya Kati ni masoko mawili makuu ya kampuni hiyo, lakini hivi sasa ana matumaini makubwa kwa soko jingine la China.

Alisema soko la China ni muhimu sana ingawa ni dogo kwa wakati huu ikilinganishwa na Ulaya, lakini kuna uwezekano wa kupanuka kwa hiyo kuna matumaini ya kuwa na wateja wengi ndani ya soko la China ambalo ni muhimu kama ilivyo muhimu maeneo ya Ulaya.

Kampuni ya Kakuzi ni ya kwanza ya wazawa kusafirisha parachichi kwenda China ingawa kuna makampuni mengi yanayopeleka bidhaa hiyo katika soko la taifa hilo kubwa la Bara la Asia.

Meneja wa Kampuni ya Sunripe inayojishughulisha na kupeleka maparachichi nchini China, Richard Wafua anasema maparachichi yanapata umaarufu mkubwa katika soko la China kutokana na ubora na kuwa na viwango vinavyostahili.

Aliiomba serikali kuangalia kiwango kikubwa cha ushuru cha asilimia saba ambacho makampuni ya Kenya yanatozwa, hali inayoifanya nchi kukumbana na changamoto ya kiushindani inapokutana na wazalishaji wa parachichi kutoka mataifa ya Peru na Mexico.

 

 

 

/* */