Kero umeme Lindi, Mtwara kuwa historia

MTWARA: SERIKALI imewasilisha mtambo  wa megawati 20 mkoani Mtwara utakaozalisha umeme kwa kutumia gesi asilia.

Mtambo huo ni utekelezaji wa ahadi ya serikali kupeleka umeme wa uhakika katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo leo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ameongoza mapokezi ya Mtambo huo aina ya TM16 wenye mfano wa injini ya ndege ya Boeing 747 utafungwa katika Kijiji cha Hiari, Wilaya ya Mtwara Vijijini.

Akipokea mtambo huo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema kuwa mtambo huo  utaondoa changamoto ya upatikanaji wa umeme kwenye Mkoa wa Lindi na Mtwara.

“Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa Wizara ya Nishati, kufanya kila jitihada ili changamoto ya umeme kwenye mikoa hiyo itatuliwe kwa haraka, tunashukuru leo tumeweza kutimiza ahadi hiyo  kwani  mtambo huu ni miongoni mwa mitambo ya kisasa kabisa ya umeme iliyowahi kuletwa nchini ambayo inatoa uhakika wa kuzalisha umeme kwa kipindi kirefu.” Amesema Mhandisi huyo.

Aidha, Mhandisi Mramba ameongeza kuwa, maelekezo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuhusu kuepeleka umeme wa gridi kwenye mikoa hiyo yameshaanza kutekelezwa ambapo kabla ya mwezi wa sita mwakani umeme wa Gridi ya Taifa utakuwa umefika kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara.

Kuhusu maelekezo aliyoyatoa Naibu Waziri Mkuu na  Waziri wa Nishati ya kuhakikisha wananchi  wa mikoa hiyo inayozalisha gesi kwa wingi wananufaika na uwepo wa nishati hiyo, amesema tayari wameanza kuboreshewa huduma mbalimbali ikiwemo kuwajengea kituo cha Polisi, ununuzi wa boti ya kisasa kwa ajili ya usafiri wa wananchi eneo la Songosongo mkoani Lindi na ujenzi wa kituo cha afya eneo la Madimba mkoani Mtwara..

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas  alisema kuwa, wananchi wa Mtwara wamepokea kwa furaha mtambo huo ambao utafungua fursa za uwekezaji kwa kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika  kwani takriban asilimia 80 ya matumizi ya umeme mkoani humo yanatumika kwenye sekta ya biashara.

Habari Zifananazo

Back to top button