Kesi ya maofisa 7 wa polisi kusikilizwa Jan 11
KESI ya mauaji inayowakabili maofisa saba wa polisi mkoani Mtwara imepangiwa tarehe nyingine ya kusikilizwa kutokana na upelelezi kutokamilika.
Watuhumiwa hao jana walifikishwa kwa mara nyingine mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara na kupangiwa kusikilizwa tena Januari 11, mwaka huu.
Walifikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Mussa Esanju.
Mara ya kwanza maofisa hao walifikishwa mahakamani Januari 25, mwaka 2022 kwa tuhuma za kufanya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamisi (25) mkazi wa Kijiji cha Ruponda, wilayani Nachingwea mkoani Lindi.
Kesi hiyo ni namba 01 ya Mauaji mwaka 2020/2022 iliyoendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Florence Mbamba.
Washitakiwa ni Mrakibu wa Polisi, Gilbert Kalanje ambaye ni Mkuu wa Upelelezi, Wilaya ya Mtwara; Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Charles Onyango ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara na Mrakibu wa Polisi Msaidizi, Nicholaus Kisinza ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara.
Wengine ni Mkaguzi wa Polisi, John Msuya; Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi mkoani Mtwara, Mkaguzi wa Polisi, Msaidizi Marco Mbuta; Mkaguzi wa Polisi, Shirazi Mkupa pamoja na Koplo Salimu Mbalu.