KESI ya kikatiba iliyofunguliwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee (Chadema) na wenzake 18, itaendelea kusikilizwa Mei 17 na 18, 2023 baada ya kuahirishwa kwa kile kilichoelezwa kuwa Jaji anayeendesha kesi hiyo, Cyprian Mkeha, yuko kwenye majukumu mengine.
Kesi hiyo iliahirishwa jana katika Mahakama Kuu Masjala Kuu na Msajili wa mahakama hiyo, Veronika Mteta aliyetoa taarifa ya kutokuwepo jaji huyo.
Itakaporejea mahakamani Mei 17, mawakili wa upande wa watoa maombi (Mdee na wenzake) wataendelea na maswali ya dodoso kwa mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Dk Lucy Mollel ambaye anahojiwa baada ya kumaliza kuhojiwa mjumbe wa kwanza, Profesa Azaveli Lwaitama.
Wabunge hao wa viti maalumu walifungua shauri kuomba mapitio ya kimahakama wakipinga uamuzi wa kikao cha Baraza Kuu la Chadema wa kufukuzwa uanachama.
Awali, wakili wa wajibu maombi wa kwanza (Chadema), Peter Kibatala aliomba mahakama iruhusu wabunge tisa kati ya 19 waliomo katika kesi hiyo waitwe mahakamani kwa ajili ya mahojiano. Wabunge wanne walifanyiwa mahojiano kabla ya Kibatala kuwasilisha hoja ya kusitisha mahojiano.
Wabunge waliohojiwa ni Hawa Mwaifuga, Cecilia Pareso, Nusrat Hanje na Jesca Kishoa huku wengine akiwemo Halima Mdee, Esther Bulaya na Esther Matiko wakiachwa.
Baada ya Chadema kusitisha mahojiano, mawakili wa watoa maombi waliomba kuwahoji Profesa Lwaitama na Dk Mollel ambapo walimaliza kumhoji Profesa Lwaitama na wanatarajia kumhoji Dk Molel.
Katika shauri hilo, wabunge hao pamoja na mambo mengine, waliiomba mahakama ipitie mchakato na uamuzi huo wa Chadema kuwafukuza uanachama, kisha itoe amri tatu.
Wabunge hao wanaomba mahakama itengue mchakato na uamuzi wa kuwavua uanachama. Pia wanaomba iwalazimishe Chadema kuwapa haki ya kuwasikiliza.
Vilevile wanaomba mahakama itoe amri ya zuio dhidi ya Spika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kuchukua hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapotolewa uamuzi.