Kesi ya ubakaji dereva bodaboda kusikilizwa Agosti 14
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam imepanga Agosti 14, 2023 kusikiliza kesi ya ubakaji inayomkabili dereva bodaboda, Chiko Muunguja anayedaiwa kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 15.
Muunguja anadaiwa kumbaka binti huyo ambaye ni shemeji yake kwa kuwa amemuoa dada yake.
Wakili wa Serikali, Daisy Makakala amedai leo mbele ya Hakimu Mkazi, Aron Lyamuya kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kusikilizwa.
Amedai kuwa shahidi mmoja ambaye ni baba wa binti aliyebakwa, Khamara Haji amefika mahakamani hapo kutoa ushahidi lakini hawezi kuendelea na ushahidi kwa sababu hajisikii vizuri.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Lyamuya alikubaliana na ombi la shahidi huyo na kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 14, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.
Katika kesi hiyo namba 192/2023 Muunguja anadaiwa katika tarehe isiyojulikana, Disemba 2021 maeneo ya Kunduchi Mtongani wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, alimbaka mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 15.
Hata hivyo, mtoto huyo ametoweka nyumbani kwao eneo la Kigamboni tangu Juni 8, mwaka huu wakati kesi hiyo imepangwa kwa kusikilizwa huku jitihada za kumtafuta zikiendelea.