Kesi ya ubakaji ya ‘P-square’ kusikilizwa upya

KESI ya ubakaji iliyokuwa ikimkabili Beach Boy, Dunia Seleman (36) maarufu Psquare imeamriwa kusikilizwa upya baada ya hukumu ya kifungo cha maisha jela kuwa na kasoro.

Awali Seleman alidaiwa kumnajisi mtoto wa miaka minane, wakati akimfundisha kuogelea eneo la Coco Beach, alihukumiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni ( Kinondoni) kutumikia kifungo hicho baada ya kukiri kosa lake.

Uamuzi wa kusikiliza upya kesi hiyo umetolewa na  Jaji John Nkwambi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala ya Dar es Salaam.

Amesema kuwa hukumu iliyotolewa  na Hakimu Mkazi Mkuu, Erick Rwehumbiza haiwezi kusimama, kwani kuna makosa yaliyofanyika katika mwenendo wa kesi hiyo.

Amesema kuna vielelezo ambavyo vilitolewa na upande wa mashitaka na kupokelewa bila kusomwa kwa mshitakiwa.

Aliongeza kuwa kwa kushindwa kufuata matakwa ya sharia: “Naondoa vielelezo vyote vilivyokubaliwa na kurekodiwa kama P1, P2 na P3 kwa sababu havikusomwa kwa mshitakiwa wakati vinapokelewa na mshitakiwa hakupewa nafasi ya kutoa maoni yake kuhusu vielelezo hivyo.”

Amesisitiza kuwa: “Ninaruhusu rufaa hii na ninafuta hukumu na adhabu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya, ninaamuru kesi kusikilizwa upya kwa Hakimu mwingine, lakini pia mshitakiwa ataendelea kuwa chini ya uangalizi wa polisi.”

Inadaiwa Agosti 13,2022 majira ya saa 9 maeneo ya Coco Beach Kinondoni, Dar es Salaam Psuare alimnajisi mtoto mwenye umri wa miaka minane.

 

Habari Zifananazo

Back to top button