SERIKALI kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo mbioni kufanya mabadiliko ya sheria kwa kuondoa dhamana katika makosa ya ubakaji na ulawiti nchini.
Hayo yamesemwa leo Februari Mosi, 2023 na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Judith Kapinga (CCM) aliyetaka kujua kama kuna mkakati wa kurekebisha sheria ili ubakaji na ulawiti kwa watoto uwe na kifungu tofauti.
Judith amesema sheria ya ushahidi iliyopo hivi sasa humpatia mtoto ugumu wa kudhibitisha kuwa amebakwa au amelawitiwa.
Akihoji Judith anasema “Je serikali haioni umuhimu wa kufanya marekebisho ya sheria ya ushahidi ili kuhakikisha mazingira ya utoaji ushahidi kwa watoto kwa kesi za ubakaji na ulawiti kwa watoto zinawekewa mazingira zinazolinda haki za watoto?
Akijibu swali hilo, Katambi amesema kuongezeka kwa matukio ya ubakaji na ulawiti kwa watoto haitokani na upungufu wa sheria.
Amesema unapoacha kuhakikisha, ushahidi unadhibitisha pasiposhaka athari yake kuwa kuna watu wanaweza wakaumizwa kwa kesi za kutengenezwa.
Katambi amesema ushahidi imeonyesha kuwa unaharibika katika ngazi ya upelelezi ambapo watoto wanafanyiwa matendo hayo lakini kunakuwa hakuna ushahidi wa ujazaji wa PF3, hivyo kuharibu kesi.
“Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 inaainisha ubakaji na ulawiti kuwa ni makosa ya jinai. Kwa mujibu wa Sheria hii, kosa la ubakaji limeainishwa chini ya kifungu cha 130 na adhabu yake imeainishwa kwenye kifungu cha 131,” amesema Katambi.
Aidha, Katambi alisema kosa la ulawiti na adhabu yake zimeainishwa chini ya kifungu cha 154 cha sheria hiyo na makosa yote mawili yanatolewa adhabu tofauti kulingana na mazingira na namna kosa lilivyotendeka.
Aliongeza kuwa adhabu ya chini kwa makosa hayo ni kifungo cha miaka 30 jela na adhabu ya juu ni kifungo cha maisha jela.
Alisema na kuwa makosa yote mawili yanapotendeka kwa mtoto chini ya miaka 10, adhabu yake ni kifungo cha maisha jela.
Pia adhabu hizo zinaweza kuambatana na kulipa fidia kwa kiwango kitakachoamuliwa na mahakama.