Kiduku ampa ushindi Dulla Mbabe

BONDIA Twaha Kassim ‘Kiduku’ amesema anampa nafasi Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ ya kushinda katika pambano la usiku wa kisasi dhidi ya mpinzani kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Erick Katompa litakalochezwa kesho Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana Kiduku alisema anaamini Dulla Mbabe atafanya vizuri kwa kuwa amejiandaa na alipata muda mzuri wa kupumzika na kujiweka imara.

“Mungu amtangulie Dulla Mbabe na naomba Watanzania tumuombee dua kwani akishinda atakuwa anaipeperusha bendera ya Tanzania,” alisema bondia huyo anayeishi mkoani Morogoro.

Kiduku alisema pambano la mwaka juzi Dulla alifanya vibaya kwa sababu hakupumzika alikuwa ametoka kucheza mapambano tofauti lakini awamu hii amepumzika vya kutosha ana kila sababu ya kushinda na kulipiza kisasi.

Pambano hilo lisilokuwa la ubingwa linatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam.

Naye promota wa pambano hilo Seleman Semunyu alisema maandalizi yamekamilika na kuhimiza mashabiki wa bondia huyo kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono.

Semunyu alisema anaamini kwa maandalizi mazuri aliyofanya Dulla Mbabe hatawaangusha Watanzania kwani amejipanga vizuri na yuko tayari kulipiza kisasi chake kwa Katompa.

Wengine watakaopanda ulingoni ni Loren Japhet dhidi ya Nassibu Ramadhan, Ramadhan Idd dhidi ya Peter Tosh, Hassan Ndonga dhidi ya Tasha Mjuaji na wengine wengi.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button