Kigahe: njooni muwekeze fursa zipo
DAR ES SALAAM: SERIKALI imewahimiza wafanyabiashara na wawekezaji wa Misri kuwekeza nchini ili kuwe na bidhaa nyingi zinazozalishwa ndani badala ya kuingiza kutoka nje.
Hayo yamesemwa leo Februari 20,2024 na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe katika Kongamano la wafanyabiashara wa Misri na Tanzania, lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema, Tanzania kuna mazingira mazuri ya uwekezaji, hivyo watumie fursa hiyo kuja kuwekeza
“Sisi kama serikali tungependa kuona wafanyabiashara mnazalisha bidhaa hapa hapa nchini kwa manufaa ya watanzania na Waafrika, ” amesema Kigahe na kuongeza
“Kwa niaba ya serikali tungependa tuone wafanyabiashara hawa wa Misri sio tu wanaleta bidhaa kutoka Misri ila wawekeze hapa waweze kuzalisha hapa Tanzania.
“Hata kwenye uzalishaji wa sukari badala ya kuzalisha huko nje na kuja kutuuzia waje wazalishe hapa, tumeona kuna haja ya kupunguza bidhaa zinazoingia Ili uptuwe na bidhaa zinazotoka kwenda soka la nje na hiyo itawezekana kama tukiwa na wawekezaji hao hapa nchini,”amesisitiza.
Aidha amesema, eneo mojawapo walilovutiwa wafanyabiashara hao ni kuona namna gani kuna ndege ya kubeba mizigo.
Nae, Mwakilishi kutoka Shirikisho la Viwanda Misri (FEI) Dk Sharif Elgabaly amesema moja ya eneo aliloguswa ni kusikia Tanzania kuna kiasi kikubwa cha gesi na kwamba inaweza kuwa na maana kwa nchi kama serikali itatengeneza mipango thabiti ya kuhakikisha inatolewa baharini kuletwa nchi kavu.
Amesema ikifanyiwa kazi inaweza kutumika kwenye viwanda huku akiongeza kuwa akilinganisha Tanzania na Misri, anaona fursa kubwa kwa Tanzania kuendelea kiviwanda kwasababu ya uwepo wa rasilimali ikiwemo ujazo mkubwa wa gesi ambao unatosha kuendesha na kusuma viwanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Gilead Teri alisema awali, kuwa lengo la kuwakutanisha wawekezaji wa pande mbili ni kuwaonesha fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuwahamasisha kushirikiana ili kufanya uwekezaji wa pamoja.
“Miaka ya karibuni uwekezaji wa Misri nchini umekuwa ukiongezeka kufuatia ziara ya Rais Samia Suluhusu Hassan nchini Misri mwaka 2021, aliyevutia kampuni kutoka Misri kuja kuwekeza, na sasa wapo wengine wamekuja kuangalia maeneo,”amesema.
Teri amesema takribani makampuni 50 kutoka Tanzania na 10 kutoka Misri yamekutana kutoka sekta mbalimbali za madawa, biadhaa za majumbani, ujenzi, miundombinu na kilimo.