Kigoma wajipanga upatikanaji maji

KIGOMA; Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Kigoma Ujiji (KUWASA), imesema kuwa imejipanga kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inapatikana kwa saa 24 kwa wakazi wa manispaa ya Kigoma Ujiji na vitongoji vyake, ikiwemo kuhakikisha kila mkazi wa mji huo anapata maji.
Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA, Poas Kilangi amesema hayo akitoa taarifa ya utendaji ya mamlaka hiyo kwa viongozi wa serikali za mitaa na watumishi wa mamlaka hiyo, wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki tano kwa watendaji wa mamlaka hiyo na kuwapongeza watendaji waliofanya vizuri.
Amesema kuwa wakati huu ambapo mradi mkubwa wa maji wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 42 ukiwa umekamilika, wanapambana na changamoto mbalimbali zinazokwamisha upatikanaji maji kwa wananchi ,ikiwemo kuchakaa kwa baadhi ya miundombinu ya kupeleka maji kwa wananchi na sasa wako kwenye hatua ya utekelezaji kuondoa changamoto hiyo.

Akielezea kukabidhiwa pikipiki tano kwa watendaji wa mamlaka hiyo zilizotokana na mapato ya ndani, amesema itatimiza azma yao ya kufanya kazi saa 24, hasa watumishi wa idara ya ufundi na miundombinu, ili kushughulikia tatizo la upatikanaji maji wakati wote, bila watendaji hao kuathiriwa na changamoto ya usafiri.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya Kigoma, Salum Kali amesema kuwa Serikali imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha inapeleka huduma kwa wananchi wak,e ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama Kigoma Ujiji, hivyo kuwataka viongozi hao wa serikali za mitaa kusaidia mamlaka katika kutoa taarifa za uvujaji wa maji unapotokea.

Kuhusu kukabidhiwa kwa vitendea kazi hivyo, amesema ni sehemu ya mpango wa serikali kurahisisha utendaji na kuwataka watumishi waliokabidhiwa pikipiki hizo kuzitumia kulingana na malengo na mpango wa mamlaka, ili kufanikisha utoaji huduma kwa wananchi.



