Kiir kukutanisha wanasiasa wa Sudan kwa suluhu
JUBA; RAIS wa Sudan Kusini, Salva Kiir amesema atakuwa mwenyeji wa wawakilishi wa kisiasa kutoka Sudan, katika jitihada za kutafuta muafaka baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe kudumu kwa miezi sita sasa.
Taarifa ya kitengo cha habari cha Ikulu ya Rais Kiir imesema kwamba kikao hicho kitafanyika jijini Juba wiiki ijayo, kikilenga kuepusha maafa na madhila ambayo wananchi wa Sudan wanapitia. Haikuelezwa ni akina nani hasa watahudhuria kikao hicho.
Kiir, kiongozi wa nchi iliyozaliwa kutoka Sudan aliwataka viongozi wa kisiasa na kijeshi kumaliza mzozo uliopo kwa majadiliano. Alikuwa akizungumza Jumatatu jioni baada ya kujadiliana na Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Sudan, Malik Agar Eyre, juu ya maendeleo yalivyo huko Sudan.
Mshauri wa kitaifa wa usalama wa Rais Kiir, Tut Gatluak Manime, amenukuliwa akisema kwamba viongozi wa Sudan watapitia tena Mkataba wa Amani wa Juba uliosainiwa 2020 kati ya serikali ya mpito ya wakati huo na waasi, kwa ajili ya kutafuta muafaka wa mzozo husika.