Kijana ahukumiwa kuchapwa viboko 24
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe imemhukumu mkazi wa kijiji cha Msia kata ya Chitete wilayani humo, Furaha Simkonda achapwe viboko 24 baada ya kumkuta na hatia ya kutaka kumbaka mwanafunzi wa darasa la kwanza mwenye umri wa miaka sita.
Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Shughuli Mwampashe alisema mahakama imemtia hatiani mshitakiwa huyo mwenye umri wa miaka 18 baada ya kujiridhisha na ushahidi wa upande wa mashitaka.
Mwampashe alisema mahakama ilitoa hukumu ya kuchapwa viboko 24 kwa mujibu wa kifungu cha sheria 160(B) cha sura ya 17 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Alisema vitendo vya ubakaji na ulawiti vimeshamiri wilayani humo hivyo adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa wenye tabia za kuharibu ndoto za watoto.
Simkonda aliomba impunguzie adhabu kwa kuwa ilikuwa mara ya kwanza kufanya kosa kama hilo na atakuwa balozi mwema kwenye jamii.
Awali, mwendesha mashitaka wa serikali, Elibariki Mpinga aliieleza mahakama kuwa kijana hiyo alitenda kosa Julai 8 mwaka huu kwa kumvamia mwanafunzi huyo majira ya saa tano asubuhi wakati akienda shuleni akiwa amevaa sare za shule.
Mpinga alidai wakati mshitakiwa akitaka kumfanyia kitendo cha kingono mtoto huyo, mwananchi aliyesikia kelele kichakani alikwenda kumuokoa mtoto.
Mahakama ilielezwa kuwa kijana huyo alikamatwa Julai 24 mwaka huu katika eneo la sokoni kwenye Kijiji Cha Msia kwa ushirikiano na wananchi baada ya kuwapo taarifa kuhusu kijana huyo kutaka kumnajisi mtoto.
Mmoja wa mashahidi katika kesi hiyo, Esinati Mtinya, aliieleza mahakama kuwa wakati akienda shambani alisikia sauti kichakani ya mtoto kulia na alipokwenda, alikuta kijana huyo amemuangusha akiwa amevua suruali mpaka kwenye magoti na alijaribu kumkamata lakini alimshinda nguvu na kukimbia.
Nje ya mahakama, Ofisa Ustawi wa Jamii wilayani humo, Tabitha Swila alisema vitendo vya ubakaji vimekithiri wilayani humo na kwamba, kesi zaidi ya tano zimefikishwa mahakamani hapo zikiwamo za kunajisi watoto wenye umri chini ya miaka 15.