MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Arusha imeamuru Ismail Sang’wa (28) anyongwe hadi kufa baada ya kumkuta na hatia ya kumuua kwa kukusudia aliyekuwa Meneja wa Ulinzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (Tanapa), Emmilya Kisamo (59).
Jaji wa Mahakama hiyo, Joackim Tiganga alitoa hukumu hiyo jana akieleza kuwa mahakama imejiridhisha kuwa Sang’wa alimuua Kisamo jijini Arusha Desemba 18, 2015.
Jaji Tiganga alianza kuisikiliza kesi hiyo ya mauaji kuanzia Februari 15 mwaka huu na alieleza mahakama imejiridhisha pasipokuwa na shaka kuwa Sang’wa alitenda kosa hilo la mauaji kwa kukusudia.
Alisema kijana huyo alimkata shingo kwa nyuma zaidi ya mara tatu na alikufa papo hapo nyumbani kwake Uzunguni jijini Arusha.
Jaji Tiganga alisema baada ya kutimiza azma hiyo, Sang’wa alimbeba na kumweka katika gari lenye namba za usajili T 435 CSY aina ya Toyota Mazda, mali ya marehemu na akaenda kumtelekeza Njiro nje kidogo Jiji la Arusha akiwa ndani ya buti la gari hilo na akarudi nyumbani Uzunguni.
Alisema hukumu hiyo pia imezingatia maelezo ya onyo aliyoyatoa Sang’wa katika kituo cha polisi kwa kukiri kufanya mauaji na kabla ya kufanya mauaji mshitakiwa alieleza kuwa alimwandalia uji wa mbege na akamwekea katika chumba cha chakula.
Jaji Tiganga aliieleza mahakama kuwa baada ya kumwandalia uji huo wa asubuhi, Sang’wa alikwenda mahali alipolificha panga na kulichukua na kumnyemelea kwa nyuma na kumkata mara tatu Kisamo akafa papo hapo.
Alisema pia hukumu hiyo imezingatia ushahidi wa mashahidi 10 katika kesi hiyo na vielelezo 24 vilivyowasilishwa na upande wa Jamhuri uliokuwa ukiongozwa na waendesha mashitaka waandamizi wa serikali, Janeth Sekule, Charles Kagilwa na Grace Madikenya.
Jaji Tiganga alieleza kuwa mashahidi walieleza namna Sang’wa alivyokuwa na nia ovu ya kumuua Kisamo na waliwasilisha vielelezo vilivyotumika katika tukio hilo likiwamo panga alilotumia kijana huyo.
Katika kesi hiyo mshitakiwa alikuwa akitetewa na wakili Victor Bernad na alikuwa na shahidi mmoja. Jaji Tiganga alisema anamhukumu Sang’wa anyongwe hadi kufa kwa kuwa aliua kwa kukusudia.