Kijana muuza barafu auawa Mpanda

Waombolezaji wakiwa msibani kwa Charles Elias

MWILI wa kijana Charles Elias (18) anayejishughulisha na kuuza barafu, mkazi wa Kata ya Makanyagio umeokotwa katika Mtaa wa Mikocheni Kata ya Kawajense Manispaa ya Mpanda, Mkoa wa Katavi ukiwa umetelekekezwa kwa kile kinachodaiwa ameuawa na watu wasiofahamika.

Wakizungumza eneo hilo Faustina Kapufi na Monica Alfonce wakazi wa Kata ya Kawajense, wamedai majira ya alfajiri waliamshwa na jirani yao kuwa nyumba ya jirani kuna tukio, ndipo baada ya kutoka wakakuta mwili wa marehemu umetelekezwa, huku wakihusisha tukio hilo na vikundi vya uhalifu vinavyofanywa na vijana wadogo walio chini ya umri wa miaka 18 viitwavyo Damu Chafu, Manyigu na Kaburi Wazi.

“Tulipofika tulimpigia simu Mwenyekiti akaja na kuangalia ikaonekana huyo kijana sio mkazi wa Kawajense, akapiga simu Polisi wakafika, wakauliza hakuna mlichokishuhudia?

Advertisement

Tukawaambia hamna purukushani yoyote tuliyoisikia, baada ya hapo walichukua mwili na kuondoka nao,” amedai Faustina Kapufi.

Naye Diwani wa Kata ya Kawajense, Uwezo Bacho amesema tukio hilo ni kiashiria cha uvunjifu wa amani ndani ya Kata hiyo, kwani hilo ni tukio la pili ambapo tukio la kwanza lilitokea la mtu kufia nyumba ya kulala wageni na kutoa wito wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria vya uhalifu.

Kwa upande wake Athuman Lumbwe, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigoma Kata ya Makanyagio, ambako ndiko nyumbani kwao marehemu amesema wamesikitishwa na tukio lililompata kijana huyo, kwani alikuwa mchapakazi na alijishughulisha na biashara ndogo ya kuuza kwa kutembeza barafu mtaani.

“Mwili wa marehemu umekutwa ukiwa umechomwa visu sehemu za mbavuni, lakini eneo ambalo mwili ulikutwa inaonekana kwamba kijana huyu hakupata ushirikiano wowote katika kuokoa maisha yake,” amesema Lumbwe.

Mama wa marehemu Ester Pigangoma amesema majira ya saa nne asubuhi ya Aprili 20,2023 , akiwa kazini alipigiwa simu na mdogo wake akimfahamisha mwanae amechomwa kisu na amefariki.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi,  Ali Hamad Makame alipoulizwa kuhusu tukio hilo amesema bado hawajapata taarifa za kina juu ya tukio hilo, hivyo watatoa taarifa baada ya kulifanyia kazi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *