Kijiji cha Wanyere waanza kujenga sekondari

WAKAZI wa Kijiji cha Wanyere, Kata ya Suguti jimboni Musoma Vijijini wameanza  kutekeleza hatua za awali za ujenzi wa sekondari, ili kunusuru wanafunzi wanaotembea umbali wa takriban Km 36 kufata elimu kwenye sekondari ya Kata hiyo na kurudi nyumbani.

Hatua hiyo pamoja na faida nyingine, itapunguza msongamano wa wanafunzi madarasani, katika Sekondari ya Suguti ambayo inahudumia wanafunzi kutoka katika vijiji vinne.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao ambao walikuwa wakisafisha eneo unakofanyika ujenzi huo, waliomba mchango kutoka kwa Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa jimbo hilo, Profesa Sospeter Muhongo na wadau wote wa maendeleo ndani na nje ya Mkoa wa Mara, ili wafanikishe azma yao.

Tayari wakazi hao kutoka vitongoji sita vya kijiji hicho wamesafisha eneo husika na wanaendelea na kazi za kusomba mchanga, mawe, huku Prof.  Muhongo akichangia  mifuko 100 ya saruji.

Kwa niaba ya wenzake, mwanakijiji Judith Chibunu alisema uamuzi wao huo utapunguzia watoto changamoto zinazotokana na kutembea mwendo mrefu kufata elimu kwenye kata, hivyo wanaamini wataungwa mkono.

Naye Kaimu Mtendaji wa Kijiji hicho, Khanifa Ibrahim alipongeza mwitiko wa wananchi katika kuchangia nguvu kazi, hali inayosababisha shughuli zote za maandalizi ya ujenzi kufanyika kwa kasi kubwa.

Michango yote kwa ajili ya kuwezesha ujenzi huo ipelekwe kupitia Akaunti Namba 30302301050, Benki ya NMB ya Kijiji cha Wanyere.

Akizungumzia ujenzi wa Sekondari jimboni humo, Prof Muhongo alisema pamoja na Kijiji hicho, Kijiji cha Muhoji na Kisiwa cha Rukuba pia ujenzi unaendelea na kwamba wamepanga shule zote hizo zifunguliwe Januari mwakani.

Habari Zifananazo

Back to top button