Kikwete akerwa wingi wachezaji wa kigeni

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amekerwa na wachezaji wa kigeni kutawala soka la Tanzania na kuishauri Serikali kukaa na TFF, Shirikisho la Soka Tanzania, kuja na mkakati wa kuzalisha wachezaji bora wazawa.

Pia amewataka wanariadha wakongwe kuangalia namna ya kufufua mchezo wa riadha, ambao kwa sasa unaonekana kudorora.

Kikwete ametoa kauli hiyo jana jijini hapa baada ya kushiriki mbio za kilomita tano za JKT Marathon, ambazo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo.

Alisema ni aibu kila siku mashabiki kuwataja wachezaji wa kigeni huku wazawa wakiwa hawapo.

“Kilio changu ni tukazanie kuinua vipaji vya wachezaji wa ndani, Yanga na Simba, kila siku  Mayele, Bangala, Diarra, Baleke, Chama, Ntibanzokiza sasa katika wale wanaosifiwa wachezaji wa Tanzania hawamo.

“Kwa sasa ukiuliza mchezaji gani maarufu Simba utasikia Baleke, utasikia kacheza mechi sita tu, Yanga kule utasikia  Mayele sasa wakiondoka?

“Hili sio jambo dogo Mwinjuma (Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo) nilisema siku moja pale kwenye sherehe za Yanga mbona mnatoa wachezaji wengi, jibu lao TFF wakaongeza kutoka wanane wakapeleka 12.

Kikwete alisema hali hiyo inasukumwa na viongozi wa klabu kubwa za Simba na Yanga ambao wanawaza ushindi tu.

“Ninyi mliopo hapa hawa wanashinda lakini katika kushinda huko wachezaji wa Tanzania nao wanashinda?

Alisema hasemi kwamba wasichukue wachezaji kutoka nje ila wajiulize kwanini wanaong’ara ni kutoka nje na wazawa hawafanyi vizuri.

“Lakini kama jukumu letu ni kushinda tu basi, mtu anasema kama unatafuta paka kwa kukamata panya huna haja ya kuchagua rangi ya paka.”

Kuhusu riadha, Kikwete alisema watanzania wanapenda soka sana kuliko riadha, lakini walioleta sifa kubwa nchini ni wanariadha na kutaka kupangwa kwa mikakati wa kufufua mchezo huo.

“Nimewahi kufanya mkutano na wanariadha maarufu nchini akiwemo Jumaa Ikangaa na kuwaambia kuwa mchezo wa riadha umedorora. Hebu kaeni shirikianeni, tumieni hiyo nguvu ya ushawishi mliyonayo maana Bayi kavunja rikodi ya dunia, Ikangaa hebu kaeni chini wekeni mikakati ya kufufua riadha.”

Bayi alivunja rekodi ya dunia ya mbio za meta 1,500 mwaka 1974 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Christchurch, New Zealand na baadae yeye (Bayi) na Suleiman Nyambui walitwaa medali za fedha katika Michezo ya Olimpiki ya Moscow 1980.

Mbali na kuweka rekodi ya dunia aliyodumu nayo kwa miaka mitano kabla ya kuvunjwa na Muingereza Sebastian Coe, Bayi aliendelea kudumu na rekodi ya Jumuiya ya Madola ya meta 1,500 kwa miaka 48 kabla ya kuvunjwa mwaka jana katika Michezo ya Birmingham, Uingereza.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa alisema JKT itaendelea kuthamini na kuendeleza michezo na tayari timu ya wanawake ya JKT Queens imekuwa bingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) huku Mashujaa ikipanda  Ligi Kuu.

Kwa upande wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda alisema jeshi litaendelea kudhamini na kuibua vipaji vya wanamichezo nchini kwa manufaa ya jeshi na nchi kwa ujumla.

Naye Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema anasikitika kwa timu yake ya Mbeya City kushuka daraja, huku akiipongeza Mashujaa kwa kupanda Ligi Kuu.

Naye Mkuu wa Jeshi la JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele alisema lengo la mbio hizo ni kulitangaza jeshi hilo na kuweka hamasa katika jamii kupenda michezo.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x