Kikwete akoshwa na miradi ya TASAF Iringa

IRINGA: Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa usimamizi mzuri katika utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF.

Amesema kupitia usimamizi mzuri wa utelekezaji wa miradi hiyo,TASAF imeweza kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii katika kaya za walengwa pamoja na wananchi katika maeneo ya utekelezaji.

Amesema hayo mkoani Iringa wakati akizungumza na Walengwa wa TASAF wa Kata ya Ruaha iliyopo katika Manispaa ya Iringa mara baada ya kukagua daraja lilojengwa katika eneo la Kingemgosi ikiwa ni utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaotekelezwa na TASAF.

Kwa mujibu wa taarifa ya TASAF Mkoa wa Iringa inaonesha kuwa jumla ya miradi 474 ikiwemo uchimbaji wa visima vya asili, utengenezaji wa barabara, uzibaji wa makorongo na kuanzishwa kwa mashamba ya korosho ilitekelezwa kati ya Julai 2022 na Juni 2023.

Pia, mkoa ulipokea  jumla ya  Sh bilioni 10.3, kati ya hizo Sh bilioni 8.9 zilitolewa kwa Walengwa 30,988 kutoka vijiji 585 wakati Sh bilioni 21.6 zilikuwa ni kwa ajili ya usimamizi  ngazi ya mkoa na halmashauri.

“Nimefarijika sana kwa namna shughuli za TASAF zinavofanyika hapa katika Mkoa wa Iringa likiwemo daraja lililojengwa katika eneo la Kigenamgosi,  haya ni matokeo ya ushirikiano thabiti kati ya uongozi wa mkoa na watendaji wote wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii,” amesema.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi mtendaji wa TASAF, Oscar Maduhu amewahakikishia na walengwa wa TASAF kuwa waendelea kubuni miradi ya kimaendeleo kwani serikali imetanga jumla ya Sh. 51 bilioni kwa ajili ya walengwa hao.

“TASAF inaendelea kuhakikisha walengwa wote wanahudumiwa ipasavyo ili kuwaondoa katika hali ya umasikini uliokithiri kupitia ruzuku,miradi ya ajira za muda pamoja na kuwapa elimu ya kuweka na kukopa katika vikundi mbalimbali,” alisema Maduhu.

 

 

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button