Kikwete anapowatolea uvivu vitatange

MWENYEKITI Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete amekemea vikali hulka ya baadhi ya wanachama wa CCM kupayuka payuka, fitna, uzandiki kwa kuendekeza mambo ya kuokoteza okoteza.

Katika salamu zake kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 10 wa CCM uliomalizika juzi Dodoma, Mwenyekiti Mstaafu amekerwa na mwenendo wa baadhi ya Wanachama wanaozungumza Kwenye vibuyu, kwenye redio mbao badala ya kutumia vikao halali.

Dk Kikwete ameeleza bayana kwamba hakuna mwanasiasa ndani ya CCM anaeweza kuchukua fomu kuwania urais mwaka 2025.

” Mhe Rais usisikilize porojo za watu, simwoni mtu wa kushindana na Samia 2025 kwanza si utaratibu wetu wala mila yetu,” alisema  Mwenyekiti Mstaafu Dk Kikwete.

Matamshi ya Mwenyekiti Mstaafu Kikwete yamewakata maini wale waliokuwa na tamaa ya fisi.

Kauli hii ya Rais Kikwete inanikumbusha wimbo maarufu Visiwani Unguja ” Mpewa hapokonyeki”.

” Aliyepewa kapewa tu hata ukifanya chuki bure unajisumbua” shairi lilitungwa na Marehemu Haji Gora katika kitabu chake cha Kimbunga ukurasa wa 35 shairi namba 39 ubeti wa kwanza na wa tatu.

Haji Gora anasema:” Aliyepewa kapewa, naapa hapokonyeki, kwa alichojaaliwa, Wallahi hapunguziki, ukimtilia nongwa unajipatisha dhiki.

” Mpewa hapokonyeki,  aliyepewa kapewa. Wa tisa humpa tisa wa moja haongezeki, alomnyima kabisa, hata akitaharuki, atabaki na kunasa, atakwama hanasuki. Mpewa hapokonyeki , aliyepewa kapewa.”

Rais Dk Samia ndio Kiongozi wetu, tumemchagua wenyewe katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 akiwa Mgombea Mwenza.

Ni kiongozi makini, mwenye imani na huruma, msikivu, mnyenyekevu na asiyependa dhulma wala kuonea watu.

Kwa hakika, matamshi ya Mwenyekiti mstaafu Dk Kikwete yananikumbusha visa na hulka ya samaki aina ya Kitatange.

Baharini kuna samaki aina ya Kitatange. Kwa wale wasiomjuwa Kitatange ni aina ya samaki mwenye umbo dogo.

Hulka yake  Kitatange ni ya ulaghai, ujanjaujanja, ambaye amekuwa akiishi katika sehemu tofauti baharini na mara nyingi anapenda kutembea peke yake.

Kwa wavuvi na watu wa asili ya upwa, mara nyingi Kitatange unaweza kumuona kwenye maji ya kina kifupi na wakati mwengine maji ya kina kirefu.

Kitatange mara nyingi hapendi kutembea na samaki wengine, ukimuona yupo na samaki wengine hapo kutakuwa na mashaka anawatafutia wenziwe.

Kitatange kwa umbile lake dogo, hawezi kunasa katika dema, hivyo huwapeleka samaki wakubwa demani akiwalaghai kufuata chakula, wakiingia demani hawatoki, yeye huyo anapita upande wa pili.

Ukidurusu kwa kina hotuba ya Mwenyekiti Mstaafu Dk Kikwete utawakuta akina Kitatange. Hawa wanaropokwa kwenye mitandao, kwenye mikutano isiyo ya kisiasa wakiaminisha watu uvumi.

Kama mnavyofahamu kuwa ni muda sasa kumejitokeza baadhi ya Wana CCM na wengine walipata kushika nyadhifa kubwa wakibeza na kukejeli jitihada za serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

Vitatange  walianza kusema chini chini, wakaanza kusema katika mitandao na wengine tunawasikia na kuwaona wakipasa sauti wakikosoa uamuzi sahihi wa serikali uliofanywa katika baadhi ya mambo kwenye mikutano ya kijamii.

Wakati wa uhai wa Rais wa Awamu ya Tano wanasiasa hawa walifunga mdomo, wengine walikuwa kama kasuku, lakini ajabu hii leo wamekuwa wakosoaji na wasemaji wakijiegemeza katika dhana ya uzalendo.

Vitatange wananikumbusha kisa cha miti na shoka. Siku moja miti  midogo ikawauliza miti mikubwa  mbona kuna hali isiyo ya kawaida tunaanza kupotea kidogo kidogo.

Miti mikubwa ikasema hakuna kitu, baada ya muda wakaanza kuona shoka likikata miti mikubwa na hapo ndipo walipotazama na kusema: ” Na wenzetu wapo.”

Mwenyekiti mstaafu hataki kuchelea yaliyowafika miti mikubwa maana mchelea mwana kulia, hulia yeye.

Watu wanaopayuka ovyo kusema yasomaana waitwa ndani ya chama na kuulizwa kulikoni.

Maana matamshi na vitimbi vyao kwa kiasi kikubwa yamenipa fadhaa na kuujaza moyo wangu shungi la masikitiko kwa kuyaona matamshi yao ya kubeza jitihada za Rais Dk Samia   ni kama yaliokosa mantiki.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button