RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuunda kikosi kazi cha ukusanyaji wa maoni kuhusu masuala ya siasa kwa kusisitiza kuwa uwepo wake utasaidia kupunguza joto la kisiasa lililopo nchini.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuwasilisha maoni katika kikosi hicho, Kikwete alisema kuundwa kwake ni kitendo cha kiungwana na busara zilizofanywa na Rais Samia kuhakikisha demokrasia inazidi kukua nchini.
“Nimefurahi nimepata nafasi ya kuja mbele ya kikosi kazi hiki, kitasaidia kupunguza joto ndani ya nchi, matumaini yake kitatusaidia kutengeneza maridhiano na mwenendo mzuri wa kufanya shughuli za kisiasa hapa nchini,” alisema Kikwete.
Kuhusu maoni aliyoyatoa mbele ya kikosi kazi hicho, Rais Kikwete alisema amejibu kutokana na alivyoulizwa na wajumbe wa kikosi hicho hivyo wao ndio wana jukumu la kuelezea kile alichowasilisha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi, Profesa Rweikaza Mkandala alisema wamefarijika kupokea maoni ya Kikwete na hasa kutokana na nafasi yake ya ufahamu wa masuala mbalimbali. Alisema wanaamini mchango wake utawasaidia kufikia lengo la jukumu walilopewa.
Alisema mbali na Rais Kikwete, kikosi hicho pia kilipokea maoni kutoka kwa viongozi mbalimbali, taasisi na wadau wengine kwa njia ya mahojiano na maandishi na kesho watamaliza kupata maoni kutoka vyama vya siasa.
Profesa Mkandala alisema kwa sasa kikosi hicho kipo katika hatua za mwisho za kukusanya maoni yake huku kikiendelea pia na kazi ya kuandaa ripoti na kwamba matarajio ifikapo mwishoni mwa wiki ijayo, kazi hiyo rasmi itakuwa imekamilika.