Kikwete awatunuku vyeti wahitimu 2,091 UDSM 

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jakaya Kikwete 

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amewatunuku vyeti wahitimu 2,091 wa duru ya tatu mahafali ya 52 wa fani mbalimbali katika chuo hicho.

Mahafali hayo yamefanyika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, ambapo kati ya wahitimu hao wa kike ni asilimia 55 na wahitimu wa kiume asilimia 45.

Akizungumza  wakati wa mahafali, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Willium  Anangisye, aliwataka wahitimu kukumbuka kwamba wameachana na ulimwengu wa masomo na sasa wanajiunga na kwenda kuishi na jamii.

Advertisement

“Mnaohitimu mmeachana na ulimwengu nwa masomo mnajiunga na kwenda kuishi na jamii ya watu wa kawaida, hivyo ni vyema muwe wepesi kujifunza mambo mapya na kubadilika kwa haraka, ili msiachwe nyuma na wakati,” amesema Profesa Anangisye.

Amesema wahitimu wanaorudi kwenye vituo vyao vya kazi, ni vyema wakaenda kuongeza tija katika majukumu yao na wakaoneshe tofauti katika utendaji na utumishi wao wa kila siku na kuwa mfano wa kuigwa kwa wanaowazunguka.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Balozi Mwanaidi Sinare, amesema, baraza linawasisitiza wanataaluma kufanya bidii katika kufanya tafiti kwenye maeneo yatakayogusa maisha ya Watanzania, ili tafiti hizo zitoe majibu ya matatizo yaliyoko katika jamii.