Kikwete: Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS itaondoa uonevu

IRINGA: NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema matumizi ya mifumo mipya ya kupima utendaji kazi wa watumishi wa umma (PEPMIS na PIPIMS) pamoja na tathimini ya rasilimali watu itaondoa malalamiko na uonevu kwa wafanyakazi serikalini.

 

Ridhiwani ametoa kauli hiyo leo Jumatatu (Desemba 18, 2023) wilayani Arumeru, mkoani Arusha, wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kukagua mafunzo ya matumizi ya mifumo hiyo yanayoendelea kufanyika mikoa yote nchini.


“Nitoe rai kwa watumishi wa umma kote nchini kuipokea mifumo hii ya TEHAMA kwa mikono miwili kwa kuwa suluhu katika usimamizi wa shughuli tunazofanya kila siku serikalini,” Naibu Waziri amesema.
Ameongeza kwua mfumo wa zamani wa upimaji (OPRAS) ulikuwa umegubikwa na udanganyifu, uonevu na upendeleo wa hali ya juu miongoni mwa watumishi.


Kutokana na hatua hiyo, Naibu Waziri amewataka watumishi wa umma nchini kufurahia ujio wa mifumo hiyo mipya kwani itatoa haki kwa watumishi wote.

Amefafanua kuwa mifumo hiyo ni suluhu ya masuala yote yaliyokuwa yakilalamikiwa na watumishi hususani suala la kupandishwa vyeo kwa wakati kwa kuwa viongozi watakuwa na uwezo wa kuona utendaji kazi wa kila mtumishi katika mfumo.

 

Katika hatua nyingine, Ridhiwani amesema mifumo hiyo mipya inakwenda kumlazimisha mtumishi kutekeleza majukumu yake kulingana na fani aliyosomea na si vinginevyo.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Zainab Makwinya amesema mifumo hiyo imekuja wakati muafaka kwani itatoa nafasi kwa watumishi kuwahudumia wananchi na sio kukaa ofisini.

Ameongeza kuwa mfumo huo utabaini watumishi wanaokwenda ofisini kusaini tu na kuondoka ili kuwahudumia wananchi.

 

Awali, Mkurugenzi wa Idara wa Usimamizi wa Maadili kutoka Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora ambaye pia muwezashaji wa mafunzo hayo, Leila Mavika amesema mafunzo ya mifumo hiyo katika Halmashauri ya Meru yamekamilika kwa asilimia 80 na wanatarajia kumaliza kwa wakati na ndani ya kipindi kilichopangwa.

Habari Zifananazo

7 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button