Kikwete: Sitaki longolongo, msiniabishe timizeni ahadi

DAR ES SALAAM: RAIS Mstaafu Jakaya Kikwete amewataka Wakuu wa Mikoa kutimiza ahadi za fedha walizotoa, kwa ajili kuiwezesha serikali kupata kiasi cha Dola za Marekani milioni 50. za sekta ya elimu.

Kikwete ametoa kauli hiyo  leo Agosti 31,2023 jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya Wakuu wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara kuahidi kuchangia jumla ya sh bilioni 465.
“Mmetoa ahadi, ahadi ni deni, Singida imeahidi  sh milioni 88, Mtanda (Mkuu wa Mkoa wa Mara) umeahidi sh milioni 100 heee! mtoe jamani, msitoe ahadi kama za Fundraising.” Amesema Kikwete na kuongeza
“Jumla ya sh milioni 465 mmeahidi,  nawashukuru sana ila msinitie aibu, msiniabishe ahadi zisiwe kama za Fundraising watu wanajitokeza ili tu wapate kupiga picha na Rais akaitumie kwenye mambo yake utasikia mtu wangu sana huyu, picha na Rais unaenda kuombea mkopo benki. ” Amesema Kikwete na kufanya waudhuriajia kuangua vicheko.
Akisisitiza anasema “Mimi ndio  Mwenyekiti wa GPE huko Dunia, leo leo napeleka ripoti tumefanya mkutano mkubwa wa Wadau wa elimu tumekusanya kiasi hiki, sasa sio upite mwezi  wa tisa, wa kumi, wa kumi na moja holaa! Desemba wanakuja;……
“Sitaki wakifika waniulize mchango wa wadau sekta ya elimu upo wapi, mtaniabisha, mtanidhalilisha sana, nitajitaidi kusema tupo kwenye mchakato, lugha ya Watanzania, Mzee mambo yanakwenda usiwe na wasiwasi. ” Anasema Kikwete na kuangua kicheko.
Katika hafla hiyo, Mkoa wa Mara umeahidi kutoa sh bilioni 155, Singida sh bilioni 88, Tanga sh bilioni 14, Njombe sh bilioni 7.8, Lindi sh bilioni 4, Shinyanga sh bilioni 5.7, Pwani sh bilioni 55.8 na Songwe sh bilioni 9.
Mikoa mengine ni Kagera imeahidi kutoa sh bilioni 6.3, Simiyu sh bilioni 6.5, Manyara sh bilioni 13.7, Geita sh Bilioni 11.4 , Arusha sh bilioni 8.3, Dodoma sh bilioni 14.5, Iringa sh bilioni 5, Mtwara sh bilioni 6.2 Katavi  sh 24.9, Kilimanjaro sh bilioni 6.7, Mbeya sh bilioni 4, Kigoma sh 5.2, Dar es Salaam sh bilioni 20, Rukwa sh bilioni 4.1, Morogoro sh bilioni 16.25, Mwanza bilioni 9.4 na Ruvuma sh bilioni 4.9
3 comments

Comments are closed.