Kila eneo la kazi kuwa na ofisa ustawi jamii

Naibu Katibu Mkuu wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Amon Mpanju

WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu imesema itakuja na mkakati wa kuweka maofisa ustawi wa jamii katika maeneo ya kazi ili kuwasaidia wanaokumbana na ukatili hasa rushwa ya ngono na ajira kwa watoto.

Katika mkutano wa siku mbili wa maofisa wa ustawi wa jamii wa mikoa uliomalizika Jumatano Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Amon Mpanju alisema hatua hiyo itasaidia kupambana na ukatili sehemu za kazi na ndani ya jamii.

“Kila mwajiri au mwekezaji iwe kwenye viwanda, migodi, taasisi za kidini, shule lazima kuwe na sharti la kuwa na ofisa ustawi wa jamii ili kuweza kuzuia ukatili kwa sababu tunaona watu wanabakwa kazini, wengine kupata ajira wanalazimishwa vitendo visivyostahili,” alisisitiza.

Advertisement

Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa ajira kwa watoto hasa katika viwanda na migodini. Alibainisha kuwa maofisa hao pia watawekwa katika taasisi za kidini kutokana na watu wengi kufika kupata ushauri baada ya kupata changamoto.

“Kwa sababu kuwa mchungaji hujasomea namna ya kukabiliana na madhila ya watu wengi; akinamama, akinababa wanakimbilia kwa viongozi wa dini ili wapate ufumbuzi, bahati mbaya wanawakuta na wenyewe wana changamoto wanachukua nafasi ya changamoto zile na kufanya yasiyostahili, hivyo lazima wafuate sheria na wasiongeze changamoto,” alieleza.

Kupitia mkutano huo, alisema wamepata maazimio 12 na lengo ni kushirikiana na wadau kuweka afua za kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu nchini kwa kuweka miongozo, kanuni na sera na mikakati kuhakikisha jamii nzima inawajibika kulea watoto katika makuzi bora.

Mpanju alisema wanakuja na mkakati wa kitaifa kuhakikisha kuwa maofisa ustawi wanakuwa na weledi, ujuzi na maarifa ya kupambana na vitendo vya ukatili katika jamii.

“Ishara ya kuwa ndoa haziko salama ni kuwapo kwa watoto mitaani na ni kweli ndoa haziko salama kama tumelegalega katika misingi ya kuandaa watu kuingia katika ndoa kwa kuwapa mafunzo sahihi, maelekezo na kuwasimamia sasa watu wanadhamini ndoa na waliodhamini wenyewe wana changamoto,” alisema.

Alibainisha kuwa wanataka kila mtu awajibike kuanzia msimamizi, mfungisha ndoa na wengine watimize wajibu wao na wapinge ukatili.