Kila la heri Burundi maonesho ya utalii EAC

BURUNDI inatarajia kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Pili ya Utalii kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EARTE) yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 23 hadi 30 mwaka huu na kuhusisha nchi zote za Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), maonesho hayo yatafanyika katika viwanja vya Circle Hippique de Bujumbura.

Imeelezwa kuwa maonesho ya 2022 yatakuwa na washiriki zaidi ya 250 kutoka nchi 10, mawakala wa kimataifa na kikanda zaidi ya 120 na pia yatahudhuriwa na wafanyabiashara zaidi ya 2,500.

Sote tunaamini kuwa maonesho ya utalii yanatoa fursa kwa sekta ya utalii kwa nchi zote wanachama kukutana na wadau mbalimbali wa sekta hiyo na kujenga uelewa kuhusu fursa za kitalii katika mataifa ya Afrika Mashariki.

Aidha, ni katika maonesho hayo tunajifunza namna ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo na namna ya kuzitatua ili kuiwezesha kuendelea kuwa kichocheo cha uchumi wa taifa kupitia mapato yake.

Kwa kuwa maonesho ya kwanza ya utalii katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika mwaka Jumatatu jijini Arusha, Tanzania yalikuwa na mafanikio makubwa, tunaamini maonesho ya Burundi yatakuwa na mwendelezo wenye manufaa makubwa kwa mataifa ya Afrika Mashariki na wenyeji wa maonesho.

Hakika nchi za Afrika Mashariki zina mambo mengi yanayofanana katika masuala ya utalii hivyo ni wakati mwingine wa kuziangalia nchi hizi na kuwa na mfumo utakaowezesha kuwa na ushirikiano wa kisekta ili kuusogeza mbele utalii wa Afrika Mashariki.

Tunaitakia nchi ya Burundi maandalizi mema ambayo yatawezesha wadau wote kuwa na utaratibu mzuri wa maonesho ambayo huunganika na makongamano mbalimbali yenye lengo la kuibua fursa na kukabili changamoto za kisekta.

Tunaamini kuwa mafanikio ya maonesho hayo si sifa tu kwa Burundi bali pia ni sifa kwa nchi zote za Afrika Mashariki kwa sababu yatachangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga na kuimarisha uchumi wa nchi zote wanachama na kwa Afrika kwa ujumla.

Mafanikio ya maonesho hayo pia yataonesha dunia kwamba Burundi kuna utulivu na amani ya kutosha kuwezesha maisha ya kawaida na ya uwekezaji.

Tunaziomba nchi wanachama wa Afrika Mashariki kuhakikisha kuwa zinatoa ushirikiano wa kutosha kwa Burundi katika kufanikisha maonesho hayo ambayo yataongeza thamani ya utalii wa Afrika Mashariki.

Habari Zifananazo

Back to top button