TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kesho inaendelea na kampeni zake za kusaka nafasi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) itakapoikaribisha Uganda au The Cranes kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Hii ni hatua ya pili kwa Taifa Stars katika mbio za kusaka kufuzu kwa fainali za Chan 2023 zitakazofanyika nchini Algeria kuanzia Januari 8 hadi Februari 5. Hizi ni fainali za saba za mashindano hayo.
Katika hatua ya kwanza, Tanzania ilifanikiwa kuiondoa Somalia na kupata nafasi ya kucheza dhidi ya Uganda ili kupata timu itakayokwenda Algeria katika fainali hizo.
Kikosi cha Taifa Stars chini ya kocha Kim Poulsen kiko kambini kwa siku kadhaa kikijiandaa kwa mchezo dhidi ya The Cranes utakaofanyika kesho Jumapili kwa Mkapa.
Ni matarajio ya wengi kuwa Taifa Stars imeandaliwa vizuri na iko tayari kuikabili Uganda na kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele na kufuzu kwa mara ya pili kucheza fainali za Chan.
Kwa mara ya kwanza, Tanzania ilicheza fainali hizi ilikuwa mwaka 2009 nchini Ivory Coast zilizopigwa kuanzia Februari 22 hadi Machi 8 na sasa inasaka nafasi nyingine ya kufuzu.
Hii ni mara ya tatu kwa Taifa Stars na Uganda kukutana katika mechi za kufuzu na kila moja imeshinda mchezo mmoja na hivyo kuonesha kuwa timu hizo zinajuana.
Katika Chan, Tanzania iliifunga Uganda mabao 3-1 katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za mwaka 2009 na The Cranes waliifunga Taifa Stars kwa mabao 4-1 kusaka nafasi ya kucheza fainali za mwaka 2014.
Mchezo dhidi ya Uganda ni muhimu, kwani ushindi wa nyumbani utaiweka Stars katika nafasi nzuri ya kupenya na kutinga fainali hiyo ya Algeria.
Benchi la ufundi limefanya kazi yake, hivyo kazi imebaki kwa wachezaji kutumia maarifa waliyopewa pamoja na juhudi zao binafsi kuhakikisha wanafuzu kwa fainali hizo.
Tunaitakia kila la heri timu yetu ya taifa ya soka, Taifa Stars, iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo.