Kila la heri Wakenya

Dk William Ruto

MAHAKAMA ya Juu nchini Kenya imetupa mapingamizi tisa yaliyowasilishwa na mgombea wa urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja, Raila Odinga na wenzake, kupinga ushindi wa Dk William Ruto aliyetangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9, mwaka huu.

Hatua hiyo imefungua njia ya mchakato wa kuapishwa kwa kiongozi huyo kuwa rais wa tano wa Kenya.

Katika kesi hiyo, Raila na wenzake waliiomba mahakama itengue ushindi wa Dk Ruto na kuamuru uchaguzi mwingine huku moja ya hoja yao ikidai kwamba Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alikiuka sheria kwa kutoshirikiana na baadhi ya makamishna wake katika ujumlishaji na utoaji wa matokeo.

Advertisement

Kutokana na kukosa ushahidi wa moja kwa moja pasi na shaka kuthibitisha madai ya walalamikaji, mahakama ya juu ilihitimisha kesi hiyo kwa kuthibitisha ushindi wa Dk William Ruto kuwa rais mteule wa Kenya.

Tunawapongeza wananchi wa Kenya kwa hatua hiyo, kwani kama alivyosema Ruto saa chache baada ya uamuzi wa mahakama, hakuna aliyeshindwa wala kushinda katika mchakato mzima wa uchaguzi kuanzia mwanzo hadi jana kwa sababu mshindi ni taifa la Kenya na wananchi wa Kenya kwa ujumla wao.

Tunatoa pongezi hizi kwa sababu Wakenya walianza mchakato wa kumtafuta Rais wa Awamu ya Tano kwa amani na utulivu na wamehitimisha safari hiyo jana kupitia uamuzi wa mahakama kwa amani na utulivu.

Tunatoa pongezi pia kwa mahakama ya juu kwa kuendesha mchakato wa kusikiliza kesi hiyo ya uchaguzi kwa uwazi kiasi cha kuwaridhisha wananchi wa Kenya na dunia kwa ujumla na hivyo mahakama za Afrika na duniani kote zinacho cha kujifunza.

Uwazi uliooneshwa na mahakama umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kumaliza uchaguzi wa Kenya kwa amani na utulivu na kuwafanya walio wengi nchini Kenya kuridhika na uamuzi huo na wale ambao pengine walikuwa wakisikia uvumi kwamba kulikuwa na wizi wa kura kuujua ukweli.

Tunawapongeza pia wanasiasa na viongozi mbalimbali wa Muungano wa Azimio la Umoja, hususani kiongozi wa muungano huo, Raila Odinga kwa kukubali na kuheshimu uamuzi wa mahakama na hata tamko lake jana kwamba timu yake itaendelea kutafuta haki tunaamini haitakuwa kwa nia ya kuvuruga utulivu uliopo.

Tunawapongeza wananchi wote wa Kenya kwa kuonesha utulivu wa hali ya juu muda wote wa kusubiri maamuzi na tunaamini utulivu utaendelea hadi Rais Mteule atakapoapishwa na kuendelea na maisha chini ya rais mpya.

Tunachukua fursa hii pia kumpongeza Rais Mteule, Ruto kwa hotuba yake ambayo kwa mara nyingine amesema serikali atakayoiunda haitalipa kisasi na iko tayari kushirikiana na wapinzani huku ikimtumikia kila mtu bila kujali dini, kabila au alimpigia nani kura.

Tunawatakia kila la heri wananchi wa Kenya katika kipindi hiki cha kuelekea kuapishwa kwa Rais Mteule, Dk William Ruto. Ni vyema sasa wote wakubaliane na kaulimbiu ya ‘Kenya kwanza’ kivitendo.

NUKUU

“Wakati ninaamua kumuunga mkono Uhuru Kenyatta, sikumpa masharti ya kuniunga mkono mimi nitakapogombea. Alipoamua kumuunga mkono mtu mwingine, simlaumu hata kidogo,” Dk William Ruto.