Kila la heri Yanga Mkutano Mkuu leo

MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara leo katika Ukumbi wa Mkutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere wanafanya Mkutano Mkuu wao wa kawaida. Mara ya mwisho Yanga walifanya Mkutano Mkuu wa Uchaguzi mwaka jana, uliowaingiza madarakani Rais wa timu hiyo, Hersi Said, Makamu wake, Arafat Hajji na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

Tunapenda kuchukua fursa hii kuipongeza Yanga kwa kufuata kalenda ya mikutano ambayo ndiyo hasa inayowaweka pamoja wahusika wote kuanzia wafanyakazi, wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kongwe hapa nchini.

Nini tunataka kuwaambia wana Yanga? Wanayanga tunawaambia kuelekea Mkutano Mkuu wa kawaida uliotishwa na uongozi wa Yanga chini ya rais wake Hersi wajadili ajenda zote kwa umakini mkubwa wakiweka masilahi mapana ya klabu hiyo kama ambavyo walifanya wakati wanawachagua viongozi hao.

Kinyume chake kitakuwa ni kuirejesha klabu hiyo kwenye migogoro mikubwa kwani nyakati kama hizi za Mkutano Mkuu mara nyingi haziiachi salama klabu zetu zote kubwa kwa maana ya Yanga na Simba.

Mara nyingi chokochoko na migogoro inaibuka kwenye nyakati kama hizi; sasa hapa wana Yanga watakaopata nafasi ya kuhudhuria Mkutano Mkuu wabebe masilahi mapana ya Yanga.

Utulivu na mshikamano uliooneshwa kipindi chote cha uongozi wa Hersi na mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi kifupi, ni ushahidi tosha kama wana Yanga watawasikiliza viongozi wao na kujadili ajenda za Mkutano Mkuu ambazo tayari wanazo kwa masilahi mapana ya Yanga basi klabu hiyo inaweza kupata mafanikio mengine makubwa. Kwa kuzingatia kauli ya “Daima Mbele, Nyuma Mwiko” na ‘Yanga kwanza, mtu baadaye’ tunaamini Yanga itakuwa na mkutano wenye ufanisi na tija hivyo kuifanya klabu izidi kusonga mbele. Kila la heri Yanga kwenye mkutano wenu mkuu leo.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button