Kilabu cha pombe Iringa kuwa soko la Samaki

HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa imeagiza kilabu cha pombe za kienyeji cha Kijiweni kibadilishwe matumizi yake na kuwa soko la samaki wabichi.

Mpango huo unalenga kutanua soko la sasa la samaki lililoko pembezoni mwa kilabu hicho maarufu kutokana na mahitaji yake kuongezeka.

Akijibu swali la Hamid Mbata ambaye ni diwani wa kata ya Kwakilosa kilipo kilabu hicho kuhusu mpango wa halmashauri kuboresha soko la samaki; Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada alisema mpango huo uende sambamba na kukihamisha kilabu hicho kwa kukipeleka sehemu nyingi.

Advertisement

“Na kwa kuwa kilabu hicho kina vyumba vingi, mbali na soko hilo la samaki kuhamishiwa humo baadhi ya vyumba vitengenezwe kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa au vyakula kwa joto baridi ili kuzuia uharibifu au kuhifadhi ubora wake kwa muda mrefu zaidi kabla havijasafirishwa kwenda kwenye masoko mbalimbali ndani na nje ya mkoa,” alisema.

Akiiagiza menejimenti ya halmashauri hiyo katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani, Ngwada aliomba taarifa ya utekelezaji wa mpango huo ifike katika kamati ya fedha ili ifanyiwe kazi zaidi.

Aidha halmashauri hiyo imeitaka menejimenti yake kutekeleza mpango wa kubadili matumizi ya machinjio ya zamani ya ng’ombe ili iwe machinjio ya kuku.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Kastor Msigala amesema mpango huo unaendelea na kwamba Sh milioni 20 zitatengwa ili uweze kutekelezwa kabla ya juni mwakani.

Msigala alizungumzia pia miradi mbalimbali katika halmashauri yake ambayo imechelewa kukamilika akisema mkakati wa kuikamilisha unahusisha juhudi za kukusanya mapato ya ndani na kwa kupitia bajeti kuu.

Aliutaja mmoja wa mradi huo ni stendi kuu ya mabasi ya mjini Iringa ya Igumbilo inayohitaji zaidi ya Sh milioni 161 kukamilishwa likiwemo jengo la kupumzikia abiria.

Wakati huo huo, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imewataka wananchi kutoa taarifa za watendaji wa kata na mitaa wanaowaomba fedha za karatasi na peni wanapokwenda katika ofisi zao kupata huduma mbalimbali.

“Ni kosa kwa watendaji hao kuomba fedha kwa wananchi ili wawape huduma. Hiyo ni rushwa kama rushwa nyingine kwahiyo ni makosa kuomba na kupokea rushwa ili utoe huduma,” alisema Mstahiki Meya.

Ngwada alisema halmashauri yake imekuwa ikitoa fedha kwa matumizi ya kiofisi kwa kata zote, fedha zinazotakiwa kusaidia shughuli kama hizo kwa watendaji wa mitaa katika kata husika.

3 comments

Comments are closed.