Kilichomuua staa wa Loliwe chatajwa

JOHANNESBURG:  FAMILIA ya muziki barani Afrika, mapema leo Jumanne Desemba 12, 2023 imeamka na taarifa za huzuni za kifo cha staa wa muziki Afrika Kusini, Zahara kilichotokea jijini Johannesburg.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Waziri wa Sanaa na Utamaduni Afrika Kusini, Zizi Kodwa, imeweka wazi kuwa mwanamuziki huyo nyota amefariki dunia akiendelea kupata matibabu ya ugonjwa wa ini ulioanza kumsumbua wiki mbili zilizopita.

Zahara ambaye jina lake kamili ni Bulelwa Mkutukana ni mtoto wa sita kati ya watoto saba wa mzee Nokhaya na mama Mlamli, alizaliwa East London, Afrika Kusini na akakulia katika mazingira ya kwaya yaliyong’arisha zaidi kipaji chake

Licha ya kuwa na umri mdogo tu, Zahara ambaye jina lake limebeba maana ya ‘maua yanayochanua’ alifanikiwa kutikisa chati za muziki ndani na nje ya Afrika Kusini, punde baada ya kuachia albamu yake ya kwanza Loliwe chini ya lebo ya TS Records, Septemba 6, 2011.

Ndani ya albamu hiyo kulikuwa na ngoma mbili Loliwe, Umthwalo na Ndiza, zilizompa umaarufu na fedha na kumfanya awe kinara kwenye chati kubwa za muziki, huku mauzo yake yakifikia nakala 210,000 ndani ya wiki nne huku wimbo Loliwe peke yake ukiuza nakala 350,000 hivyo kufanya albamu hiyo iwe ya pili kwa mauzo ikifuatana na ile ya marehemu Brenda Fassie aliyewahi kufikisha mauzo ya nakala 500,000.

Mrembo huyo mwenye miaka 36, alifanikiwa kuachia albamu yake ya pili inayoitwa Phendula ikiwa na ngoma kama Phendula, Impilo na Stay ambayo haikuwa maarufu sana kama Loliwe.

Aliachana na uongozi wa lebo yake ya TS Records na kusainiwa na lebo kubwa zaidi duniani ya Warner Music na hapo akaachia albamu ya tatu inayoitwa Country Girl mwaka 2015 na albamu yake ya nne iliyotoka 2017, Mgodi ambayo ilifanikiwa kimauzo na kupewa hadhi ya platinum.

Zahara aliwahi kuweka rekodi katika mtandao wa iTunes, baada ya kuachia albamu yake ya sita, Nqaba Yam hivyo kumfanya azidi kuwa kinara kwenye muziki barani Afrika.

Mbali na mafanikio ya albamu zake, Zahara amewahi kushinda tuzo kadhaa ndani na nje ya Afrika Kusini kama vile South Africa Music Awards, Three Metro FM Awards, Next Generation Entertainment Awards, Nigeria Entertainment Awards huku akipewa heshima ya kuwa jaji mwalikwa katika mashindano 17 ya Idol South Africa 2021 na alikuwamo kwenye orodha ya wanawake bora 100 wa BBC.

Miongoni mwa nyakati ngumu alizowahi kupitia Zahara enzi za uhai wake ni pale ambapo mdogo wake wa mwisho wa kiume kuuawa, tukio hilo lilimsababishia msongo mkubwa wa mawazo (Depression) huku ndugu wa karibu wakidai hali hiyo imemfanya awe mlevi kupindukia.
Kifo cha Zahara kimewagusa mastaa kibao wa Afrika wakiwemo wasanii wa Tanzania ambao wametoa salamu zao za pole kupitia mitandao ya kijamii huku mwili wa msanii huyo ukitarajiwa kuzikwa hivi karibuni nyumbani kwao.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button