Kilimanjaro Premium Lager Marathon yazinduliwa Dar

Mbio za kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon kwa mwaka 2023 zimezinduliwa jijini Dar es Salaam leo tayari kwa tukio hilo muhimu katika kalenda ya riadha duniani linalotarajiwa kufanyika Februari 26, 2023. Hili ni toleo la 21 tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Klilimanjaro, Mhe. Nurdin babu, ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Edward Mpogolo, alisema Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zimepata muamko mkubwa na kwamba Maadhimisho ya miaka 21 tangu kuanzishwa kwake ni taswira halisi ya jinsi waandaaji na wadhamini walivyo makini na tayari kujitolea ili kufanikisha mashindano hayo.

“Tunajivunia mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, TIGO Kili Half Marathon na Grand Malt Fun Run, kwani matukio makubwa ya kimataifa katika ukanda wa Afrika Mashariki ambayo huitangaza Tanzania kwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya 12,000 kutoka nchi takribani 55, haya ni mafanikio makubwa sana”, alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Alisema mbio za Kilimanjaro Marathon zimeendelea kutoa mchango mubwa katika kukuza sekta ya utalii kwa kupitia utalii wa michezo na hivyo kuungana na Serikali katika kukuza sekta ya utalii nchini.

“Nawapongeza wadhamini wote wakiongozwa na mdhamini mkuu Kilimanjaro Premium Lager, Tigo -21km Half Marathon na Grand Malt -5 km Fun Run kwa mchango wenu mkubwa, bila nyinyi na wafadhili wengine wote pamoja na washiriki, mafanikio haya yasingeonekana”, alisema na kutoa wito kwa washiriki Watanzania kujiandaa na mashindano hayo ya kimataifa ili kuhakikisha zawadi nyingi zinabaki nyumbani.

Mkuu wa Mkoa pia alitoa wito kwa washiriki na mashabiki kutumia msimu wa Marathon kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii miongoni mwao vikiwemo Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Ngorongoro, Zanzibar na vivutio vingine.

Aliwapongeza wadhamini wa mashindano hayo ambao alisema ni pamoja na Simba Cement, Kilimanjaro Water, TPC Sugar, na wasambazaji rasmi GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel na CMC Automobiles.

Kwa upande wake, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi, ambaye pia ni Meneja wa Chapa ya Grand Malt, alisema wao kama wadhamini wakuu wanajivunia kuwa sehemu ya mafanikio katika sekta ya michezo hapa nchini kupitia Kilimanjaro Marathon, ambayo amesema ni tukio kubwa ambalo kwa kutimiza miaka 21 limechukua muda mrefu tangu kuanzishwa kwake.

“Kwa miaka yote hii kupitia mashindano haya tunayodhamini tumesaidia kwa kiasi kikubwa kuhamasisha michezo hususan maendeleo ya riadha, ukuaji wa sekta ya utalii na utamaduni kwa ujumla hapa nchini”, alisema.

Meneja huyo aliendelea kusema kuwa wamejipanga vyema kwa ajili ya mashindano ya 21 ya Kilimanjaro Premium Lager Marathon ambapo wametenga shilingi milioni 22,760,000 kama zawadi ya fedha huku washindi wa kwanza kwa upande wa wanaume na wanawake wakitarajiwa kupata zawadi ya fedha zenye tahamni ya shilingi milioni 4.2 kila mmoja.

Alitoa wito kwa washiriki kujiandikisha mapema pale usajili wa mbio hizo kupitia mtandao utakapofunguliwa Oktoba 24, mwaka huu, ambapo alisema watakuwa na fursa a kujisajili kupitia mtandano wa www.kilimanjaromarathon.com na kupitia TigoPesa kwa nambari *149*20#. Aidha alitoa wito kwa washiriki wa kilomita 5 (Mbio za kujifurahisha) kujiandikisha mapema kwani idadi ya washiriki imepangwa kuwa ndogo.

Pia alitoa wito kwa wadhamini wenza ma mashindano hayo kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki mbio kama vikundi vya kitaasisi ambapo watapata kukimbia kama kikundi na waandaaji watahesabu muda wao wa wastani na kutangaza washindi baada ya mbio. “Hii ni njia ya kipekee ya kutuleta pamoja kama wafanyakazi na pia kuhimiza usawa na mtindo wa maisha mzuri kwa ujumla,” alisema.

Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Tigo, Woinde Shisael alisema, “Kama Telco, tumekuwa wadhamini wa Tigo Kili Half Marathon kwa mwaka wa 8 kutokana na ukweli mashindao haya yamekuwa ni jukwaa muhimu katika kukuza vipaji, uchumi wa taifa pamoja na uhifadhi wa mazingira hususan maeneo ya Mlima Kilimanjaro”.

Alisema Tigo inajivunia kuwa mmoja wa wadhamini wa mashindano hayo yenye hadhi ya kipekee, ambayo alisema yanaendelea kukua kila mwaka huku yakiteka hisia za washiriki wengi wakiwemo wanariadha mahiri wa kimataifa kutoka sehemu mbalimbali duniani.

“Washiriki wanaotaka kubadilishana matukio, mandhari na uzoefu wa Tigo Kili Half Marathon – 2023 wanapaswa kujiandikisha kupitia Tigo Pesa na kupata nafasi ya kujishindia zawadi nzuri katika kampeni inayoendelea ya Wakishua Twenzetu Qatar na Hisense,” alisema.

Waandaaji wa hafla hiyo walitoa wito kwa washiriki kuchukua fursa ya punguzo la ada ya kiingilio lijulikanalo kama Early Bird kuanzia tarehe 24 Oktoba hadi usiku wa manane tarehe 15 Desemba ambapo, baada ya hapo viingilio vitaendelea kuwa vile vya kawaida ambavyo alisema havitakuwa na punguzo na kwamba tiketi zitaendelea kuuzwa kati ya Desemba 16, 2022 hadi saa sita usiku tarehe Februari 6, 2023 au pale idadi ya washiriki wa kipengele hicho itakapotimia.

Kwa upande wao waandaaji wamesisitiza umuhimu wa washiriki kujisajili mapema ili kuwezesha taratibu za maandalizi kama vile usafirishaji kwa ajili ya ufuatiliaji, usimamizi kwa ujumla, maji na viburudisho vingine, zifanyike mapema kulingana na idadi ya washiriki ziwezekufanyika mapema kwa kuzingatia idadi ya washiriki.

Aidha waandaaji hao walisema tukio hilo litakwenda sambamba na utoaji misaada kwa shirika la hisani la Tumaini la Maisha (TLM) lenye lengo la kuwafikia watoto nchini Tanzania wanaougua ugonjwa wa saratani ili waweze kupata tiba zenye ubora.

Kupitia juhudi mbalimbali za Kuinua Mfuko huo, idadi ya michango iliyotolewa na washiriki na wahisani wengine binafsi wa kujisajili mtandaoni, Kili Marathon 2022 ilikusanya karibu dola za Marekani 10,000 na fedha hizo zilikabidhiwa kwa Kituo cha Matibabu ya saratani cha Kilimanjaro [KCMC] cha Moshi, ili kusaidia huduma kwa watoto wanaougua Saratani.

“KCMC ni mshirika muhimu wa mbio za Kilimanjaro marathon kutokana na msaada wake wa kimatibabu wakati wa mashindano haya tangu mwanzo na eneo la kumalizia kila mwaka na huduma za njiani wakati wa mashindano haya”, ilisema taarifa hiyo ya waandaaji.

Washiriki binafsi na wale wa mashirika wanahimizwa ‘Kukimbia kwa Sababu’ ili kuchangisha pesa au kutoa michango ya moja kwa moja ili kuleta mabadiliko katika maisha ya watoto hawa jasiri. Maelezo zaidi yanaweza kupatikana mtandaoni kwenye tovuti rasmi ya www.kilimanjaromarathon.com

Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zitakazofanyika Jumapili Februari 26,2023 katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), zimeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions Limited.

Habari Zifananazo

Back to top button