BODI ya Mkonge Tanzania (TSB), imewatoa hofu watanzania wanaotaka kujikita kwenye kilimo cha zao la Mkonge kuhusu fursa mbalimbali ikiwemo masoko.
Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhamasishaji wa Bodi, David Maghali amesema hayo alipokuwa akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na wadau mbalimbali waliotembelea katika Banda la TSB kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam maarufu Sabasaba 2023.
Wadau hao walitaka kujua kama mtu mmoja mmoja au mkulima mdogo anawezaje kujikita kwenye kilimo hicho na fursa za masoko.
Akijibu maswali hayo Maghali amesema “Mtu yeyote anaweza kulima Mkonge kwa usaidizi wa Bodi tunaweza kumpa ushauri wa kilimo bora na kumuunganisha na masoko, soko la Mkonge lipo na ni la uhakika ndani na nje ya nchi.
”Amesema na kuongeza
“Mahitaji ya Mkonge kwa sasa ni makubwa kutokana na fursa zake na bidhaa zinazozalishwa kutokana na zao hilo lakini lakini pia kufanya tafiti mbalimbali,” amesema.
Watu wamejitokeza katika Banda hilo la TSB lililopo katika Ukumbi wa Katavi (Katavi Hall) mkabala na Banda la Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupata elimu na kujifunza Kilimo cha Mkonge na fursa mbalimbali zinazotokana na zao hilo na sekta nzima kwa ujumla.