Kilimo cha umwagiliaji sasa kwa computer
Ni teknolojia iliyobuniwa na Veta Moshi
WANAFUNZI wa mwaka wa tatu Chuo cha Mkoa VETA Moshi, mkoani Kilimanjaro wamebuni mfumo wa kisasa wa umwagiliaji mashamba na bustani kupitia kompyuta (Programmed Irrigation System).
Akielezea mfumo huo katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba, Dar es Salaam, Mwalimu Ombeni Tarimo amesema mashine hiyo sio tu ya kumwagilia maji ila pia humwagilia dawa na ni ya kwanza nchini.
“Kupitia zile taarifa anazotupa mkulima, tunaziweka kwenye kompyuta kisha tunazibadilisha katika lugha maalumu itakayotafsiriwa na chombo chetu (PLC) kisha kitaanza kufanya kazi kwa namna na idadi ambayo mkulima alitaka iwe kupitia taarifa alizotoa awali.” Amesema Tarimo
Aidha, amesema mashine inayotumika katika mfumo huo wa umwagiliaji unaruhusu aina tofauti za vyanzo vya nishati ili kuiendesha.
“Mfumo huu una njia mbili za nishati, umeme lakini pia umeme wa mionzi ya jua (solar) pia una uwezo wa kumwagilia dawa za kuua vijidudu kwenye mimea,”amesema.
Tarimo, amesema dhamira ya mradi huo ni kumsaidia mkulima kujiongezea kipato pia kumpunguzia gharama za uendeshaji
“Kupitia huu mfumo haina haja ya kuajiri watu kwaajili ya kumwagilia, mashine hii itakupunguzia gharama hizo kwani inafanya shughuli nyingi kwa wakati mmoja.”Amesema
Aidha, Tarimo ameiomba serikali kupitia programu ya kuwawezesha vijana kupitia kilimo BBT ‘Building a Better Tomorrow’ ikiwapendeza kuona haja ya kushirikiana nao katika kufanya tafiti ya mradi huo ili kuleta tija kupitia kilimo cha umwagiliaji.