Kilio cha abiria stendi ya Magufuli chasikilizwa

Kilio cha abiria stendi ya Magufuli chasikilizwa

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ameagiza kuondoa kwa katazo lililokuwa likizuia mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi kupakia au kushusha abiria katika vituo binafsi.

Makalla ameruhusu abiria wapande au kushuka katika vituo binafsi kwa sharti la kila basi liingie ndani ya kituo kikuu cha mabasi cha Magufuli.

Alitoa uamuzi huo Alhamis wakati wa kikao  kilichowakutanisha baadhi ya wamiliki wa mabasi hayo chini ya chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Usafiri Ardhini (LATRA) na uongozi wa Manispaa ya Ubungo.

Advertisement

Kikao hicho ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa kwa Makalla kwamba akutane na wadau hao ili kupata ufumbuzi wa malalamiko ya abiria.

Makalla aliridhia uwepo wa vituo vitano binafsi vilivyokidhi vigezo vya utoaji huduma baada ya kuhakikiwa na Latra na akafungua milango kwa wamiliki wengine wanaohitaji kuwa na vituo binafsi kushirikiana na Latra ili wapatiwe vigezo na leseni.

Vituo vilivyoruhusiwa kutoa huduma kwa abiria ni pamoja na cha kampuni ya mabasi ya Kilimanjaro, Dar Lux, Dar Express, ABC na Kimbinyiko.

Sehemu ya vigezo vilivyotajwa ni pamoja na uwepo wa sehemu ya kukaa abiria, choo, uwepo wa huduma za viburudisho na maegesho ya mabasi.

Makalla pia aliiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ikae na wamiliki wa stendi binafsi ili kuona njia bora ya ukusanyaji wa mapato na kuondoa malumbano.