Kilio cha wavuvi Mwanza chamfikia Kinana

WAVUVI wa Mikoa ya Mwanza na Mara, wamewasilisha kilio chao kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, wakilalamika kuwa tozo za serikali katika sekta hiyo zinawapeleka kwenye umasikini.

Pia wavuvi wamekumbushia operesheni sangara iliyofanyika mwaka 2018 na kuomba serikali iwalipe fidia, kwani iliwasababishia umasikini mkubwa, ambao haulezeki, wakati ilishakir kukosea.

Hata hivyo Kinana alionesha mshangao kuhusu utitiri wa kodi hizo na kuahidi kufikisha kilio chao kwa wahusika, ili waweze kuwasikiliza na kuwasaidia.

“Tunapozungumza sekta binafsi wengi wanafikiri viwanda vikubwa au matajiri wanaotoka nchi jirani, sekta binafsi ni hii,” alisema Kinana na kuongeza:

“Tozo ya maegesho kwenye maji? Yaani Kodi ya packing imebidi nicheke,” alisema na kuangua kicheko.

“Ndugu zangu, hizi tozo 11 niliziziona kwenye hii ripoti yenu kweli ni nyingi sana katika biashara, nitawasilisha kwa wahusika na hatua zichukuliwe, lengo la Rais Samia ni kuleta unafuu kwenye maisha ya wananchi na kuileta nchi pamoja, “amesema.

Awali katika taarifa iliyotolewa na wavuvi hao kwenye mkutano kati yao na Kinana, walisema wana maumivu makubwa ya kodi 11 wanazotozwa, hivyo wakaomba jambo hilo liangaliwe, kwa kuwa linawafanya waishi kwa umasikini zaidi.

Msemaji wa wavuvi hao,  Sijaona James, alitaja mambo 14 ambayo yanawaumiza wavuvi, likiwemo ushuru mwingi na mazingira ya utendaji kazi wao yanayotokana na baadhi ya watendaji kuwa ni miungu watu.

Alisema changamoto nyingine inayowakabili ni rushwa, uuzaji holela wa mabondo, ulinzi na usalama sio rafiki.

Alisema uvuvi kwa sasa umekuwa mwiba mchungu usioelezeka, lakini wanahisi kama watu waliosahaulika kuyafaidi matunda ya serikali yao, japokuwa wanalo tumaini kubwa kupitia Makamu Mwenyekiti wa CCM, kwamba kilio chao kinapelekwa mahali sahihi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam mstaafu, Said Mecky Sadick, akizungumza kwa niaba ya wafugaji wa samaki aliomba serikali itupie macho sekta hiyo, kwa kuwapa ruzuku ya chakula cha samaki, ili kuwapunguzia makali ya ufugaji.

Alisema: “Wenzetu wa kilimo wamepewa ruzuku kubwa tu katika mbolea, ili waweze kulima kwa wingi, sisi tunaomba ruzuku katika chakula, garama ni kubwa kati ya asilimia 40 na 50 ya operesheni ya ufugaji inachukuliwa na chakula,” amesema.

Akizungumzia Operesheni Sangara, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, alisema licha ya operesheni hiyo kuwa na upungufu,  lakini ni wazi ziwa Victoria ilikuwa inaenda kuwa jangwa kutokana na uvuvi haramu.

“Mwaka 2015 nilishiriki kuandaa Ilani ya CCM, operesheni Sangara mimi naijua, haikua ndani ya ilani, naijua kwa vile nilikua Mkuu wa Mkoa wa Mara.

“2018 tatizo la uvuvi haramu lilikuwepo na lilikua bomu lililosababisha ziwa kuwa jangwa, mtazamisha nyavu samaki hamna, na viwanda vingi vikubwa vya samaki vilikufa kwa sababu hii,” alisema.

Hata hivyo alisema operesheni hiyo, kama Mkuu wa Mkoa  hakushirikishwa hadi mambo yalipotibuka na kusisitiza kuwa yaliyofanywa ni yao na si kweli kuwa walikua wakitekeleza ilani ya chama.

Malima akijibu madai yao ya kulipwa fidia alisema: ” Mnataka mlipwe fidia, hasara ile tunaitambuaje? Tunafanyaje tathmini?”

Naye Waziri wa Ardhi, Angelina Mabula akizungumza kwa niaba ya Waziri Mifugo na Uvuvi, alisema Wizara hiyo imetengewa bajeti ya Sh bilioni 266 katika mwaka wa fedha 2022/2023 ,ambapo sekta ya uvuvi imepata asilimia 65 ya fedha.

Alisema amezichukua changamoto zote zilizotolewa na anaziwasilisha kwa Waziri husika kwa ufumbuzi.

“Changamoto zenu nimechukua na nitaziwasilisha kwa Waziri husika, kwa sababu muda mwingine watendaji wanafanya maamuzi yao kinyume na inavyotakiwa, badala yake wanaigombanisha serikali na wananchi, ” alisema Mabula.

Habari Zifananazo

Back to top button