Kilo 23.84 za Dawa ya Kulevya zateketezwa
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) leo Februari Mosi, 2023 imeteketeza kilo 23.84 za dawa ya kulevya aina ya mirungi.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya , Florence Khambi amesema dawa hizo zilikamatwa Januari 26,2023 katika operesheni maalum iliyofanyika katika wilaya ya Temeke mkoani wa Dar es Salaam.
Amesema operesheni hiyo walifanikiwa kukamata kiasi hicho cha dawa aina ya mirungi zikiwa zimehifadhiwa ndani ya nyumba ya Rhoda Mohamed Salum (48) ambaye ni mkazi wa Lukongo eneo la Wiles wilayani Temeke akiwa anajiandaa kuzisafirisha kwenda nje ya nchi.
“Aidha, January 27, 2023 katika dampo la Kituo cha Polisi Chang’ombe, kiasi hicho cha dawa za kulevya kiliteketezwa chini ya uangalizi wa baadhi ya wadau kutoka taasisi zinazotambulika kisheria kama ilivyoelekezwa kwenye Kanuni ya 14 ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.”Amesema
Ametaja washiriki hao ni pamoja na mwakilishi wa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, mwakilishi wa Inspekta Jenerali wa Polisi, mwakilishi wa Mkemia Mkuu wa Serikali, mwakilishi kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka Nchini.
Amesema, uteketezaji huo ulifanyika kuendana na matakwa ya kifungu cha 36(1) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ambacho kinaruhusu uteketezwaji wa baadhi ya dawa za kulevya kwa kuzingatia hali ya hatari ya dawa hizo, kuharibika kwake, athari za kimazingira, ufinyu wa mahali maalum pa kuhifadhia au kwa kuzingatia masuala mengine yanayofanana a hayo.
Aidha, amesema kwa kuwa mirungi hiyo ilikuwa mibichi, kulikuwepo na uwezekano mkubwa wa kuharibika na kupoteza uhalisia wake hivyo ilikuwa ni muhimu kuteketezwa kwa dawa hizo.
“Upelelezi wa shauri hili bado unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.”Amesema