Kilo 276 za dawa ya kulevya zanaswa Iringa
Watu 12 mbaroni
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, imefanya operesheni maalum katika Mkoa wa Iringa na kufanikiwa kukamata jumla ya kilo 276 za dawa za kulevya aina heroin na bangi na kuwakamata jumla ya watu 12 wakihusishwa na dawa hizo.
Akitoa taarifa kwa niaba ya Kamishna Jenerali leo Agosti 27, 2023 Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa Mamlaka hiyo Daniel Kasokola amesema kuwa lengo la operesheni hizi ni kuvunja na kusambaratisha mitandao yote ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kuwakamata wote wanaojihusisha kwa namna yoyote na dawa za kulevya ili wachukuliwe hatua za kisheria.
“Operesheni hizi ni moja ya utekelezaji wa mkakati wa kudhibiti upatikanaji wa dawa za kulevya (Supply Reduction), hivyo kama Kamishna Jenerali anavyoeleza operesheni hizi zitafanyika nchi zima.
” Tuwahakikishie tutawakamata vinara wote wanaojihusisha kwa namna moja au nyingine na kilimo au biashara ya dawa za kulevya kwani mitandao yao na mbinu zao tunazijua hivyo hakuna mhalifu wa dawa za kulevya ambaye ataukwepa mkono wa sheria. ” Amesema
Aidha, amesema serikali imejipanga kikamilifu kukabiliana na dawa za kulevya nchini, hivyo, kwa sasa Tanzania siyo sehemu salama kwa wote wanaojihusisha na biashara au kilimo cha dawa za kulevya.
Amewasihi Watanzania kuungana na serikali katika mapambano hayo kama walifanya wananchi wa Kisimiri juu, Lesinoni na Lenglong mkoani Arusha na wananchi wa walaya ya Same mkoani Kilimanjaro kuamua kwa hiari yao kuondoa mimea ya bangi na mirungi katika maeneo yao.
Pia, amesema kuwa, Dawa dawa za kulevya zina madhara makubwa kwa Taifa zikiwemo za kiafya, kijamii, kiuchumi, kiusalama na kidiplomasia.
“Nawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya juu ya watu wanaojihusisha na kilimo na biashara ya dawa hizi za kulevya kupitia njia mbalimbali ikiwemo kupiga simu ya bure namba 119.” Amesema
Amesema, katika kukahakikisha dawa za kulevya zinazibitiwa, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015 inatoa adhabu kubwa kwa wale watakaotiwa hatiani kwa makosa hayo, adhabu yake inaweza kufikia kifungo cha maisha cha miaka 30 jela hadi kifungo cha maisha pamoja kutaifishwa kwa mali zote za mshtakiwa ambazo zitathibitika alizipata katika kipindi cha miaka 10 tangu akamatwe.
Akizungumzia operesheni hiyo Mtendaji wa kata ya Malolo wilaya ya Kilosa Fredinand Litweka ameshukuru kufanyika kwa operesheni hiyo katika maeneo hayo kwani yameshamiri kwa kilimo cha bangi na kuongeza kwamba, uongozi wa wilaya umekuwa wakifanya jitihada kadhaa bila mafanikio hivyo, kufika kwa mamlaka katika maeneo yao kumeongeza chachu ya mapambano dhidi ya kilimo na biashara ya dawa za kulevya.
Nao wakazi wa Ruhaa Mbuyuni, akiwemo Jefari Jeda wameeleza kuwa, wanaunga mkono jitihada za serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kusisitiza kuwa jitihada zaidi zifanyike kuhakikisha wanawakamata wote wanaojihusisha na kilimo au biashara ya dawa za kulevya kwani madawa haya yana madhara makubwa. Wameeleza kuwa, wako tayari kutoa ushirikiano kwa serikali kwa kutoa taarifa juu ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kuonesha mashamba yaliyolimwa bangi.