Kilogramu 200 za Heroin zakamatwa

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama imefanya operesheni katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro na Arusha na kufanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 200.5.

Operesheni ya udhibiti na ukamataji dawa za kulevya kwa sasa inaendeshwa Kimataifa ambapo mataifa mbalimbali duniani yanaendelea kushirikiana kuhakikisha dawa hizo zinatokomezwa. Hivi karibuni mamlaka nchini India zilikamata zaidi ya kilo 200 za heroin ambazo zilikuwa zinavushwa kutoka Jammu na Kashmir na walanguzi wa dawa hizo hatari kwa afya, uchumi na maisha ya binadamu.

Sambamba na bangi kavu iliyokuwa tayari kusafirishwa gunia 978, bangi mbichi gunia 5,465, bangi iliyosindikwa (skanka) kilogramu 1.5 na methamphetamine gramu 531.43.

Dawa zingine za kulevya zilizokamatwa ni heroin kete 3,878, cocaine kete 138, mililita 3,840 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Pethidine pamoja na kuteketeza hekari 1,093 za mashamba ya bangi.

Hayo yamebainishwa leo Juni 19, 2023 jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akitoa taarifa ya ukamataji wa dawa hizo mbele ya waandishi wa habari.

Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa, pia kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCB) mamlaka hiyo imezuia kuingia nchini jumla ya kilogramu 1,507.46 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutengeneza dawa za kulevya.

“Ukamataji huo ulifanyika kuanzia Machi 25 hadi Juni 19, 2023 ambapo unahusisha watuhumiwa 109 wakiwemo raia watatu wa kigeni.

“Baadhi ya watuhumiwa wamefikishwa mahakamani na wengine wanatarajiwa kufikishwa mahakamani taratibu za kisheria zitakapokamilika,”amebainisha Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button